Na Francisca Swai-Mahakama, Musoma
Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Marline Komba amewapongeza watumishi wa
Mahakama ya Wilaya Rorya kwa utendaji kazi mzuri na utunzaji wa mazingira.
Mhe. Komba alitoa pongezi
hizo tarehe 27 Machi, 2023 alipofanya ziara ya kuzitembelea Mahakama za Mwanzo
na Mahakama ya Wilaya Rorya ili kukagua shughuli mbalimbali za kimahakama na
kujionea mazingira ya utendaji kazi.
Jaji huyo alimpongeza
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Rorya, Mhe. Tumaini Marwa kwa
jitihada kubwa za kutunza mazingira na kuwahimiza watumishi wote kuendelea
kuchapa kazi licha ya uchache wao.
Ilibainika kuwa katika
kipindi hiki cha mvua wamefanikiwa kupanda jumla ya miti 1,200 kwenye Mahakama
zote za Mwanzo na Wilaya Rorya ikiwa ni sehemu ya kulinda mipaka ya maeneo ya Mahakama.
Aidha, Jaji Komba pamoja
na msafara wake walifanikiwa kutembelea mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo
Kinesi uliotakiwa kukamilika mwezi Oktoba 2022 na kumsisitiza Mkandarasi PEK
Brothers kukamilisha mradi huo mapema ili jengo hilo la kisasa lianze kutumika
katika kuwahudumia wananchi.
Naye Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Moshi aliwapongeza Mahakimu
kwa namna wanavyosikiliza mashauri na kuyamaliza kwa wakati. Aliwaasa kuendelea
kufanya kazi kwa upendo na umoja.
Kwa upande wake, Mtendaji
wa Mahakama katika Kanda hiyo, Bw. Festo Chonya aliwapongeza watumishi kwa uadilifu,
hasa katika makusanyo ya maduhuli na kuwaasa waendelee kuwa makini kwa
kujiridhisha iwapo malipo yamepokelewa kabla ya kukata stakabadhi.
Jengo linalotumika kwa sasa kwa ajili ya shughuli za Mahakama ya Mwanzo Kinesi.
Mwonekano wa jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Kinesi.
Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Marline Komba (katikati) akiwa katika picha ya
pamoja na watumishi wengine mbele ya jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Kinesi. Wengine ni Naibu Msajili, Mhe. Frank Moshi (wa tatu kushoto), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama
ya Wilaya Rorya, Mhe. Tumaini Marwa (wa pili kushoto), Mtendaji wa Mahakama
Kanda, Bw. Festo Chonya (wa tatu kulia) na wengine.
Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Marline Komba pamoja na msafara wake wakikagua
maeneo ya Mahakama ya Mwanzo Riagoro.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Marline Komba, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Kanda ya Musoma pamoja na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Riagoro.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni