Na Charles Ngusa-Mahakama, Geita
Msajili Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma hivi
karibuni alifanya ziara katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita kwa lengo la
kukagua eneo linalopendekezwa kujengwa Mahakama Kuu katika Mkoa wa Geita.
Katika ziara hiyo, Mhe
Chuma aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza,
Mhe. Chiganga Tengwa na kupokelewa
na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita na Mahakimu ya Wilaya Geita.
Baada ya kupata taarifa
za awali, Msajili Mkuu aliendelea na ziara yake ya kukagua eneo hilo ili kuona
kama lina sifa zinazohitajika na miundombinu iliyopo.
Kadhalika, Mhe. Chuma alitembelea
jengo la Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu ambalo litatumiwa kwa muda na Mahakama ya
Hakimu Mkazi. Pia alikagua eneo lililokuwa likitumiwa na Halmashauri ya Wilaya
Geita, ambapo Mahakama ya Mwanzo na Mahakama ya Wilaya Geita zitahamia hapo katika
zoezi zima la kupisha ujenzi wa Mahakama Kuu.
Akiongea na watumishi
baada ya kutembelea maeneo hayo, Msajili Mkuu aliwahimiza viongozi walioshiriki
mafunzo ya mfumo mpya wa usimamizi wa mashauri (advanced case management)
kuwafundisha maafisa wa Mahakama kwa kuwa wao ndiyo watakuwa watumiaji wa mfumo
huko kwa asilimia kubwa.
Mhe. Chuma pia alihimiza
watumishi kuendelea kufanya kazi kwa weledi na bidii. Naye Naibu Msajili aliahidi
kutoa elimu aliyoipata kwa walengwa wote.
(Habari
hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Msajili Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akiwa katika picha ya pamoja na viongozi
wengine wa Mahakama, akiwemo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Mwanza, Mhe. Chinganga Tengwa (wa pili kushoto).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni