·Jaji Chaba ahimiza utekelezaji bora, ufanisi wa mfumo makazini
·Aonya uzembe, ulevi, utovu wa nidhamu
Na
Faustine Kapama`– Mahakama, Morogoro
Mafunzo ya siku tano yaliyokuwa
yanafanyika mjini hapa, kuhusu mfumo mpya wa
kielekroniki (e-complaint) wa Sema na Mahakama unaotumika kutoa na kupokea maoni, maulizo na
malalamiko (mrejesho) kutoka kwa wananchi, yamehitimishwa leo tarehe 10 Machi,
2023.
Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messeka Chaba alihitimisha mafunzo hayo yaliyokuwa
yanatolewa kwa Naibu Wasajili, Watendaji, Maafisa Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) na watumishi wengine wanaojihusisha na kupokea malalamiko
kutoka Kanda zote za Mahakama nchini kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu
Kanda hiyo, Mhe. Paul Ngwembe.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Mhe. Chaba alielezea matarajio yake kuwa mafunzo hayo yamewawezesha
kuutumia vema mfumo huo na kutoa huduma bora zaidi kwa wateja kwa kuzingatia
matumizi sahihi ya muda, kwa maana ya kuyashughulikia malalamiko kwa wakati na
kuhakikisha changamoto binafsi kama uzembe, ulevi, utovu wa nidhamu katika
kuwajibika haziathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Kuweni waalimu wazuri na
mahili kwa wenzenu ambao hawajapata fursa ya kuhudhuria mafunzo haya na hasa
mzingatie kuwa moja ya malengo ya mafunzo haya ni pamoja na kupata wakufunzi
kwa watumishi wengine wa Mahakama ya Tanzania,” alisisitiza.
Amesema kuwa anafahamu
maafisa TEHAMA ndio wenye jukumu kubwa la kwenda katika Kanda zao kuhakikisha
mfumo unaanza kufanya kazi na wanawafundisha vizuri watakaokuwa wanautumia.
“Niwaombe mtakapokwenda
katika vituo vyenu mkawe mstari wa mbele kuhakikisha mfumo wa kisasa wa
kielektoniki wa Sema na Mahakama unafanya kazi kwa ufanisi kwa kuzingatia
viwango vinavyokubalika,” alisema.
Akiwasilisha neno la
shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake, Bi.Catherine Francis kutoka Mahakama
Kuu Songea aliushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kuandaa mafunzo hayo
ambayo yamewawezesha kupata maarifa kwenye maeneo muhimu katika muktadha mzima
wa utoaji haki, hususan mfumo wa Sema na Mahakama. Ameahidi kwa niaba ya
wenzake kwenda kueneza elimu waliyoipata kwa watumishi wenzao katika vituo vyao
vya kazi.
Kabla ya kuhitimishwa
mafunzo hayo, washiriki walipitishwa kwa mara nyingine na Afisa kutoka
Kurugenzi ya TEHAMA, Bw. Lazaro Sanga namna mfumo wa Sema na Mahakama
unavyofanya kazi kabla ya kupokea “dozi” nyingine kutoka kwa Afisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Jumanne
Muna.
Akiwasilisha mada kuhusu
mbinu za ufundushaji Bw. Muna aliwaeleza kuwa watakapoenda kwenye vituo vyao
watahitajika kuwafundisha watumishi wenzao ili wajue jinsi mfumo wa Sema na
Mahakama unavyofanya kazi, hivyo wanapaswa kujua nini wanachokifundisha na namna
ya kufikisha ujumbe unaotakiwa.
“Tunafanya hivi kwa lengo
mahususi ya kuandaa wakufunzi watakaopeleka elimu waliyoipata kwa watumishi
ambao ni wengi zaidi. Tukifuata utaratibu huu tutaweza kutumia fedha kidogo,”
alisema na kuwakumbusha washiriki hao kuwa wanapaswa kutumia mbinu mbalimbali
za kufundisha kulingana na mazingira.
Amesema kuwa utoaji wa mafunzo kwa wafanyakazi ni sehemu muhimu ya ukuaji
na mafanikio katika taasisi kwani watumishi waliofunzwa vyema wana tija na huleta
ufanisi zaidi katika majukumu yao, hivyo kutoa mchango mkubwa.
Afisa Utumishi huyo alibainisha kuwa aina tofauti za mbinu za ufundishaji huja
na faida, changamoto na malengo tofauti.
“Kuna aina tofauti ya kujifunza kulingana na watu tofauti, kuna wale wanaoelewa
polepole, wengine wanahitaji sauti ya juu na wengine wanahitaji mwalimu wa
kuwaongoza. Ili wale mnaowafundisha waweze kukuelewa mnahitaji kuelewa mbinu ya
kutumia kuwafundisha,” alisema.
Mahakama ya Tanzania
imeanzisha mfumo mpya wa Sema na
Mahakama ili kurahisisha njia za uwasilishaji wa maoni na
kuongeza uwazi katika kushughulikia maoni, malalamiko na kuweza kukusanya
taarifa sahihi kutoka kwa wananchi na wadau.
Mfumo huo ambao haujajengwa
kwa ajili ya kupokea malalamiko pekee, bali pia mwananchi ana uhuru wa kutoa
maoni, mrejesho, mapendekezo au pongezi umeletwa ili kuimarisha mawasiliano
kati ya Mahakama na mwananchi kuhusu huduma zinazotolewa katika mchakato mzima
wa utoaji haki.
Kwa kupitia mfumo huu, ambao
umekamilika kwa asilimia 98 na unaweza kuanza kutumika, mwananchi anaweza
kuwasilisha maoni, malalamiko au pongezi kwa Mahakama aidha kwa kutumia simu
yake mwenyewe, kwa kuandika ujumbe mfupi au kwa kupiga na anaweza kwenda kwenye
mfumo wenyewe kwa kupitia kompyuta yake au njia ya e-mail na kuliwasilisha.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba akizungumza na washiriki wakati wa kufunga mafunzo ya mfumo wa Sema na Mahakama leo tarehe 10 Machi, 2023 katika Ukumbi wa Magadu mkoani Morogoro.
Naibu Msajili kutoka Idara ya Usimamizi na Ukaguzi wa Shughuli za Kimahakama na Maadili, Mhe. Kinabo Minja akimkaribisha Jaji Chaba kuhitimisha mafunzo hayo
Afisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Jumanne Muna akisisisitiza jambo alipokuwa anawasilisha mada kwa washiriki kabla ya mafunzo hayo kuhitimishwa.
Mwashiriki kutoka Mahakama Kuu Songea, Bi.Catherine Francis akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake.
Wajumbe wa Sekretarieti waliokuwa wanaratibu mafunzo hayo wakikamilisha kazi za mwisho mwisho.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo (juu na chini) wakikabidhiwa vyeti na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messeka Chaba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni