Na. Eva Leshange-Mahakama, Singida
Mahakama ya Hakimu Mkazi
Singida na Mahakama ya Wilaya Singida jana tarehe 9 Machi, 2023 zilikutana na wadau
katika kikao cha kusukuma mashauri ya jinai na madai kujadili namna ya kuondokana
na mlundikano
Kikao hicho ambayo
kiliongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe.
Allu Nzowa kilihudhuliwa na Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya Manyoni na
Iramba, wakuu wa taasisi za Serikali katika Mkoa, ikiwemo TAKUKURU, Magereza,
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mkuu wa Upelelezi na Mganga Mkuu.
Kwenye kikao hicho, wadau
hao walisisitiza kasi ya umalizaji wa mashauri iendane na kesi zinazofunguliwa
ili kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati. Kikao hicho pia kimeweka mikakati
mbalimbali kuhakikisha mashauri ya mlundikano yanapungua katika ngazi zote za
Mahakama na kuzuia kuwepo mahakamani.
Baadhi ya mikakati
iliyowekwa ni pamoja na kutoahirisha mashauri kwa muda mrefu, usuluhishi upewe
kipaumbele na wadau kuelimishwa, Video Conference itumike ipasavyo hasa kwa
mashahidi wa mbali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka iongeze kasi ya kutoa vibali kwa
mashauri yanayohitaji kibali hicho kabla ya kusikilizwa.
Mikakati mingine ni kutekeleza
ipasavyo muongozo wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) katika usikilizaji wa
mashauri kwa kuzingatia muda ulioelezwa wa kusikiliza mashauri na kuwa na
“clean up session” kila baada ya miezi ya mitatu kwa kutenga mwezi mmoja wa kusililiza
mfululizo mashauli yote yaliyopo katika mlundikano na yale yanayo karibia.
Aidha, waendesha mashtaka
wameomba kuwe na mawasiliano baina yao, mawakili wa kujitegemea na Mahakimu,
hasa katika kupeana taarifa za shauri limefikia muda gani toka kufunguliwa na
kuweka alama tambuzi kwa yale yote yanayo karibia kuingia kwenye mlundikano ili
kuyapa kipaumbele.
Kadhalika madaktari
wamekumbushwa kujaza fomu za PF3 kwa wakati sio hadi mgonjwa apone ili kuepuka jalada
kukaa katika hali ya upelelezi kwa muda mrefu.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni