Na Faustine Kapama –Mahakama, Morogoro
Mafunzo
ya siku 28 kuhusu Haki Jinai yaliyokuwa yanafanyika katika Kituo Jumuishi cha
Utoaji Haki Morogoro mjini hapa kwa washiriki 250 ambao ni waendesha mashtaka na wapelelezi waliotoka
taasisi mbalimbali nchini yamehitimishwa leo tarehe 24 Machi, 2023.
Naibu
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) anayeshughulikia Mipango,
Fedha na Utawala, Prof. Fatihiya Massawe amehitimisha mafunzo hayo yaliyokuwa
yanatolewa kwa washiriki kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la
Polisi, Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori na Kitengo cha
Kudhibiti Fedha Haramu.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Prof. Massawe aliwahimiza maafisa hao kuendelea kushirikiana
wanapotekeleza majukumu yao kwani hatua hiyo itaharakisha upatikanaji wa utoaji
haki kwa wananchi na kuboresha haki jinai.
"Mahakama
inaamini sana katika ushirikiano na wadau kwenye jukumu lake la kikatiba la
utoaji haki na hili linaonekana kwenye Mpango Mkakati wa Mahakama
(2020/21-204/25), hususani katika nguzo yake ya tatu. Hivyo, nitoe rai kuwa
muwe na ushirikiano wa dhati na Mahakama ili muweze kufanikisha jukumu la
upatikanaji wa haki," alisisitiza.
Aidha,
Prof. Massawe aliwaeleza kuwa mafunzo waliyopata yawe chachu ya utayari wa
kutamani kujifunza kwa kusoma uamuzi mbalimbali unaotolewa na Mahakama ambao
unaelekeza taratibu muhimu za kuzingatia katika upelelezi na uendeshaji wa
mashtaka. Alisema kwa kufanya hivyo kutawawezesha kuendelea kuongeza ujuzi mpya
utakaowawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kuibuka wakati
wa upelelezi au uendeshaji wa mashtaka.
Awali,
akimkaribisha mgeni rasmi kuongea na wahitimu wa mafunzo hayo, Kaimu Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Livin Lyakinana
alieleza kuwa Mahakama ya Tanzania inaendelea na utekelezaji wa Mpango Mkakati
Awamu ya Pili (2020/21-2024/25 na inatekeleza mradi wa kuimarisha upatikanaji
haki unaomlenga mwananchi.
Alisema
mpango huo unatekeleza maeneo makuu ya maboresho, ikiwemo uwajibikaji na
usimamizi bora wa rasilimali, upatikanaji na utoaji haki kwa wananchi na
kuimarisha imani ya wananchi na ushirikishwaji wa wadau.
"Kwa
kawaida, Mahakama imekuwa ikishirikiana na wadau wa haki jinai katika majukwaa
mengine yakiwemo vikao vya kamati za kusukuma mashauri. Mafunzo haya
yamefanyika lengo likiwa, (pamoja na mambo mengine) kupanua wigo wa azma ya
Mahakama ya kushirikiana na wadau," alisema.
Akiwasilisha
neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake,Wakili wa Serikali Sara Amandus
alisema kuwa katika mafunzo hayo wamejifunda mada mbalimbali zikiwemo za
kiuchunguzi, kuendesha mashtaka, utunzwaji wa vielelezo, ulinzi wa watoa
taarifa na mashahidi, ushirikiano kwenye ukusanywaji wa ushahidi, urejeshwaji
wa watuhumiwa, matumizi ya TEHAMA kuelekea Mahakama mtandao, hali ya mifumo na
miundombinu pamoja na maadili katika uchunguzi na uendeshaji wa mashauri.
"Mafunzo
haya yametuongezea weledi na motisha ya kufanya kazi kwa umakini, maadili
pamoja na kuzingatia maendeleo ya sayansi na teknolojia katika uchunguzi na
kuendesha kesi mahakamani. Tunashukuru waandaaji, yaani Mahakama ya Tanzania
pamoja na Chuo cha Uongozi wa Mahakama kwa kuandaa mafunzo haya," alisema.
Mwakilishi
huyo alimhakikishia mgeni raismi kuwa wanaenda kuwa mabalozi wazuri na kuwapa
elimu wale ambao hawajapata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo. Alitoa rai
kuwa mafunzo hayo yawe endelevu kwani yanawaongezea ari ya kutekeleza majukumu
yao.
Kabla
ya kuhitimishwa mafunzo hayo, washiriki katika kundi la nne walipitishwa kwenye
mada mbili, ikiwemo mikakati na mbinu za uendeshaji wa mashitaka na masuala ya
kimaadili ya uchunguzi na mashtaka, zilizowasilishwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Divisheni ya Biashara, Mhe. Awamu Mbagwa.
Akiwasilisha
mada hizo, Mhe. Mbagwa aliwahimiza waendesha mashtaka kuandaa mashtaka kulinga
na ushahidi uliokusanywa na wapelelezi na kuacha uzembe wanapoandaa na kuongoza
mashahidi mahakakani.
Aliwaeleza
washiriki hao wa mafunzo kuwa mchakato wa haki jinai hupitia hatua muhimu tatu,
zikiwemo uchunguzi unaofanywa na wapelelezi, uendeshaji wa mashtaka unaofanywa
na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na hatua ya kusikiliza na uamuzi inayofanywa na
Mahakama.
“Ili
haki ionekane imetendeka lazima hatua hizi zitekelezwe na watu watatu tofauti.
Kila hatua ina umuhimu wake katika mnyororo mzima wa utoaji haki. Hatua zote
hizi ni muhimu na lazima wanaohusika wafanye kazi yao vizuri. Tatizo huja pale
mmoja kati ya hawa anapojiona siyo muhimu. Wote wanaumuhimu sawa, tukifanya
hivyo tutawatendea haki wananchi,” alisema.
Aliwaeleza
kuwa mahusiano kati ya wapelelezi na waendesha mashtaka yasiishie pale jalada
linapowasilishwa Ofisi ya Taifa Mashtaka. Aliwahimiza maafisa hao kuendelea
kushirikiana hadi shauli lililowasilishwa mahakamani litakapohitimishwa.
Kadhalika,
Mhe. Mbagwa aliwasihi kuishi maadili wanapotekeleza majukumu yao, ikiwemo
kutumia madaraka yao vibaya na kujiepusha na kufanya vitendo vya rushwa. “Haya
madaraka ni dhamana. Kuna maisha baada ya hapa, nawaomba mzingatie maadili
kwani ni muhimu katika
mfumo wa utoaji haki,” alisisitiza.
Aliwashauli
kujitahidi kadri inavyowezekana kutoshughulikia mashauri ambayo wanamaslahi
nayo ili kuruhusu haki siyo tu itendeke bali pia ionekane imetendeka. Aidha,
aliwahimiza wapelelezi kutunza siri na kutovujisha taarifa walizozikusanya kwa
watu wasiohusika ili kulinda taswila yao wenyewe na taasisi wanazotoka.
Kwa
kipindi cha wiki nne, washiriki hao wa mafunzo walipitishwa kwenye mada
mbalimbali na walipata
nafasi ya kubadilishana uzoefu kuhusu utendaji kazi wao wa kila siku, ikiwemo
changamoto zinazotokana na kukua kwa teknoloji na kubadilika kwa mbinu za
uhalkifu na wahalifu.
Kuandaliwa kwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji
wa maboresho ya Mahakama ambayo yanatekelezwa kupitia Mpango Mkakati wake wa
miaka mitano (2021-203/2024) na ni utekelezaji pia wa Sera ya Mafunzo ya Taifa
2003 pamoja na Sera ya Mafunzo ya kimahakama 2019.
Mafunzo
hayo yaliyofadhiliwa Benki ya Dunia kupitia mradi wa maboresho awamu ya pili
yaliandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na IJA. Yalifunguliwa na
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe
tarehe 27 Februari, 2023.
Akizungumza
wakati anafungua mafunzo hayo, Mhe. Ngwembe aliwahimiza waendesha mashtaka na
wapelelezi hao kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa vile Mahakama haiwezi
kufanya maajabu, ikiwemo kumtia hatiani mhalifu kwa kuletewa shahidi dhaifu.
Alisema
jamii huwa haiielewi Mahakama pale inapomwachia mtuhumiwa aliyekamatwa na
wananchi wakishuhudia akitenda kosa. Aliwaeleza washiriki hao wa mafunzo kuwa
katika mazingira hayo, chombo kinacholaumiwa ni Mahakama, jambo ambalo
halipendezi mbele ya macho ya jamii.
“Lakini
Mahakama ifanye nini kama hakuna ushahidi wa kuweza kumhusisha mtuhumiwa na
uhalifu anaotuhumiwa nao? Kama upande wa mashtaka umeshindwa kuleta mashahidi
wa msingi, Mahakama ifanye miujiza gani? Lakini pia, upande wa mashtaka
utaendesha vipi shauri kama upelelezi haukufanywa kama inavyotakiwa? Mwisho wa
yote, mchakato mzima wa haki jinai utakuwa kituko mbele ya jamii,” alisema.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Livin Lyakinana akieleza jambo katika hafla ya kuhitimisha mafunzo hayo.
Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Bi. Fatuma Mgomba akitoa maelezo ya utangulizi katika hafla hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni