Na Arapha Rusheke-Mahakama, Dodoma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, jana tarehe 20 Machi, 2023 alifanya ziara ya kikazi ya Mahakama katika Gereza Kuu Isanga jijini
hapa kukagua
shughuli na maeneo mbalimbali.
Hii ni mara yake ya kwanza kufanya
ziara hiyo tangu ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo tarehe 8 Oktoba, 2021, kuchukua nafasi
iliyoachwa wazi na mtangulizi wake, Mhe. Dkt. Jaji Eliezer Feleshi aliyeteuliwa
kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mhe. Siyani alipokelewa na Mkuu wa
Magereza ya Mkoa wa Dodoma, Bi. Bertha Minde aliyeambatana na mwenyeji ambaye ni
Mkuu wa Gereza la Isanga. Akiwa katika ofisi ya Mkuu wa Gereza hilo, Jaji Kiongozi
alipokea taarifa ya magereza yote ya Mkoa wa Dodoma na baadae kupewa taarifa
fupi ya Gereza Kuu Isanga.
Baada ya hapo, Mhe. Siyani alikagua maeneo
mbalimbali ya Gereza, ikiwemo vyumba wanavyolala wafungwa, Zahanati ya ndani ya
gereza, jikoni kunakopikwa chakula na akamalizia ukaguzi wake kwenye kiwanda
cha kufuma vikapu vinavyotokana na mkonge.
Baadaye aliwatembelea kwa nyakati
tofauti tofauti mahabusu na wafungwa wa kiume na wa kike wa makosa ya kawaida pamoja
na wale waliohukumiwa kunyongwa na kufanya nao baraza.
Katika matukio hayo, Jaji Kiongozi alipokea
risala zao na kusikiliza hoja mbalimbali, changamoto na maswali ambayo baadhi aliyajibu
na kutoa maelezo mafupi.
Akizungumza baada ya ziara hiyo,
Mhe. Siyani alieleza kuwa haki ya wafungwa na mahabusu haikamilishwi na taasisi
moja, hivyo kila moja inatakiwa kufanya shehemu yake ili kuhakikisha wanapata
haki zao kwa wakati.
Jaji Kiongozi aliwapa pole kwa kuwa
hakuna mtu anayependa kukaa gerezani na kuwasihi wale watakao bahatika kutoka
kwa namna yeyote ile kutofanya mambo ambayo yatawarudisha tena huko.
Katika ziara hiyo, Jaji Kiongozi
aliambatana na viongozi wa Mahakama ya Tanzania kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe Wilbert Chuma, Msajili wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Shamillah Sarwatt, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Dodoma, Mhe Dkt. Adam Mambi, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Bw. Sumera
Manoti pamoja na viongozi wengine.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni