Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe amesisitiza suala la uadilifu katika jamii hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na wimbi kubwa la tuhuma za ubakaji.
Mhe. Ngwembe ameyasema hayo leo tarehe 20 Machi, 2023 wakati akifungua mafunzo ya wadau wa Haki Jinai awamu ya nne ikiwa ni muendelezo wa mafunzo hayo ambayo yalifunguliwa tarehe 6 Machi, 2023. Amewasihi wadau hao kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa weledi kwa mujibu wa taaluma zao, huku akiinyooshea kidole sekta ya upelelezi.
Kauli hiyo imekuja mara baada ya kuwa na wimbi kubwa la tuhuma za ubakaji katika jamii ambapo Mhe. Ngwembe amesema mara nyingi kesi hizo zinatokana na jamii kutokuwa waadilifu, ikiwemo baadhi yao kuzitumia kama nyenzo ya kukomoana kwa kuwa hupelekea mtu kufungwa muda mrefu gerezani.
Aidha, Jaji Ngwembe alisema kuwa upelelezi yakinifu wa kisayansi ukitumika utarahisisha kuwatambua waharifu wa ukweli katika kesi za ubakaji ili wawajibishwe na wasio waharifu waachiliwe kuendelea na majukumu yao.
Pia alisisitiza wanaopelekewa majukumu ya kupeleleza kesi hizo kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa weledi kwakuwa wakishindwa kufanya hivyo huwa chanzo cha lawama kwa Mahakama kuwa imeshindwa kutenda haki. “Sasa hivi matukio ya ubakaji yamekuwa kama wimbo katika jamii, niwaambie wazi kuwa vitendo hivi vya kinyama havikubaliki,” aliongeza.
Kuhusu upande wa upelelezi, Mhe. Ngwembe alisisitiza upelelezi wa kisayansi utumike kuutambua uhalifu kwani sasa ni karne ya 21 ambayo masuala ya tekinolojia yameshika hatamu, hivyo ni vyema wote wakahama kutoka utaratibu wa kizamani ambao umepitwa na wakati na kujikita katika tekinolojia mpya ili iwasaidie kupambanua uharifu.
“Msitumie utaratibu wa zamani, tumieni upelelezi wa kisayansi kutambua uharifu na Sheria ya Ushahidi wa Kielektroniki (Electronic Evidence Act) tayari imepitishwa na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania itumike,” alisisitiza Mhe. Ngwembe.
Sambamba na hilo, Mhe. Ngwembe aliwataka washiriki kuzingatia mafunzo yatakayotolewa na wawezeshaji na kuyatumia kuunda fikra mpya zitakazoleta mageuzi katika majukumu yao.
Awali, akimkaribisha Jaji Mfawidhi kufungua mafunzo hayo, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe, Arnold Kirekiano alitoa takwimu kuwa wameweza kuwafikia wadau wa Haki Jinai kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (50), Jeshi la Polisi (100), TAKUKURU (40), TAWA (35), Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (16) na washiriki 9 kutoka kitengo cha kupambana na fedha haramu.
Washiriki wa mafunzo hayo watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu haki jinai, lengo likiwa kuongeza ufanisi katika sekta ya utoaji haki.
(Habari hii
imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni