·
Washiriki
kujengewa weledi na umahiri katika eneo hilo
·
Watakaofaulu
kupata cheti cha kuwawezesha kuomba kazi hiyo
Na. Innocent Kansha - Mahakama
Naibu Mkuu
wa Chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto (IJA) Bw. Goodluck Chuwa leo tarehe 20 Machi, 2023 amefungua mafunzo kwa watu 27 wenye nia ya kufanya kazi ya
udalali na usambaza nyaraka za Mahakama, washiriki wa mafunzo hayo ni kutoka maeneo
mbalimbali ya Tanzania.
Akifungua
mafunzo hayo ya kundi la 10 toka kuanzishwa kwake yanayofanyika katika Taasisi
ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo jijini Dar es Salaam, yanayoendeshwa na IJA kwa muda wa wiki mbili. Bw. Chuwa amesema,
mafunzo yanayotolewa
ni sehemu ya maboresho ya Mahakama yenye lengo la kujenga weledi na umahiri kwa
wadau hao na hivyo kupunguza malalamiko na kujenga taswira nzuri ya
Mahakama mbele ya umma.
“Msingi na
msukumo wa uendeshaji wa mafunzo haya unatokana na malalamiko ya wadau wa
Mahakama yanayoelekezwa moja kwa moja kwa madalali na wasambaza nyaraka za
Mahakama dhidi ya ukosefu wa maadili na weledi katika utekelezaji wa majukumu
yao”, alisema Chuwa
Aidha, Bw.
Chuwa alisema, washiriki watakapomaliza mafunzo hayo na kuhitimu kisha
kusajiliwa na Mahakama kutekeleza majukumu ya udalali na usambazaji nyaraka za
Mahakama wataisaidia Mahakama kutenda haki kwani nafasi hizo watakazozitumikia
zitaongeza imani ya wananchi kwa Mahakama.
“Niwasihi kuwa baada ya
kupata mafunzo haya, kufuzu mitihani yenu mkafanye kazi mkitanguliza uadilifu kwa kuzingatia
kanuni na maadili mliyofundishwa ili kukidhi kiu ya Mahakama ya kuwahudumia
wananchi kwa kutoa haki kupitia wadau wengine ikiwemo madalali na wasambaza
nyaraka za Mahakama”, Chuwa alisisitiza.
Akifafanua moja ya malengo ya kuazisha progamu hiyo, mgeni rasmi huyo alisema, kuanzishwa kwa mafunzo ni mojawapo ya zao la maboresho makubwa yanayoendelea katika mhimili wa Mahakama wenye lengo la kuondoa malalamiko mengi yaliyokuwepo kutoka kwa wananchi na moja ya eneo lenye kulalamikiwa ni ukosefu wa uadilifu wakati wa utekelezaji wa majukumu ya udalali na usambazaji wa nyaraka za Mahakama, kwa kufanya hivyo kutawawezesha Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama kufanya kazi kwa uadilifu na kufuata kanuni zilizopo.
Bw. Chuwa aliongeza kuwa, ni vizuri kutambua kuwa uamuzi wa kuanzisha mafunzo hayo ya wenye nia ya kufanya kazi ya udalali na usambaza nyaraka za Mahakama ni kutokana na changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama wenye sifa na hivyo Mahakama kupitia Mpango Mkakati wake wa kwanza wa mwaka 2015/2016 – 2019/2020 na Mradi wa Uboreshaji wa Mahakama kupitia mradi wa huduma zinazomlenga mwananchi, iliandaa kanuni ziitwazo Kanuni za Uteuzi, Gharama, Malipo na Nidhamu za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kwa Tangazo la Serikali Namba 363 la 2017 (The Court Brokers and Process Servers (Appointment, Remuneration and Disciplinary) Rules, GN. 363 of 2017).
Kanuni hizo zilitoa maelekezo kwamba, madalali na wasambaza nyaraka za Mahakama wanapaswa kusoma kozi za muda mfupi ambazo itawapa weledi katika kufanya kazi ya udalali na usambaza nyaraka kwa ufanisi.
Chuwa alifafanuwa kwa washiriki hao kuwa, watajifunza mambo mengi sana katika kipindi hicho cha wiki mbili, yakiwemo masuala ya muundo wa Mahakama ya Tanzania, utaratibu wa mashauri ya madai, usambazaji wa nyaraka za mahakama, utekelezaji wa tuzo na amri za Mahakama na maadili ya madalali na wasambaza nyaraka za mahakama na nyinginezo.
“Ninawasihi
watumieni wawezeshaji wenu ambao ni Jaji
wa Mahakama ya Tanzania, Naibu Wasajili na Mahakimu ambao ni wabobevu, wazoefu na mahiri katika eneo la
sheria na taratibu za udalali na usambaza nyaraka za Mahakama kuibua
mijadala huru itakayowasaidia kuongeza ujuzi na Msisite kuchangia uzoefu wenu kwa
lengo la kuongezeana maarifa”, Chuwa
aliwashauri washiriki hao
Washiriki hao,
watafundishwa na wataalamu wabobezi na mwisho wa siku watapewa mtihani na wale
tu watakaofaulu ndiyo watapewa cheti kitakachowawezesha kuomba kazi hiyo
Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kutokana na
msingi huo, kundi hili la watu wenye nia ya kufanaya kazi ya udalali na
usambazaji wa nyaraka za Mahakama ni la kumi (10) tangia mafunzo ya namna hiyo
yazinduliwe na hadi kufikia sasa jumla ya washiriki 262 wamedahiliwa kwa
mafunzo hayo na washiriki 141 wamefaulu na kufuzu kigezo cha kuomba kazi ya udalali na
au usambaza nyaraka za Mahakama.
Mmoja wa washiriki wa
mafunzo hayo wanaotoka maeneo mbalimbali nchini azungumza na wanahabari kuhusu matarajio yao juu ya mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo hayo wanaotoka maeneo mbalimbali nchini wakimsikiliza mgeni rasmi hayupo pichani wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo wakiwa kwenye vikundi vidogo vidogo wakijadiliana maswali waliyopewa na Mkufunzi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni