·Yaizabua TEMESA bao nne, yakwea nafasi ya kwanza
Na
Faustine Kapama-Mahakama
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu imeng’ara
katika Bonanza lililoshirikisha timu tatu, zikiwemo Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Wakili FC baada ya kuibuka
vinara kwa kuzoa pointi nne na mabao matano.
Katika Bonaza hilo lililofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya
Sheria kwa Vitendo (Law School) Dar es Salaam, timu ya Wakili FC ilishika
nafasi ya pili baada ya kupata pointi nne na magori manne, huku TEMESA ikiburuza
mkia kwa kupata pointi moja na magori mawili.
Kulikuwepo na mechi tatu zilizoshirikisha timu hizo ambapo mechi
ya kwanza ilikuwa kati ya Wakili FC na TEMESA na Wakili FC kuibuka washindi kwa
mabao 3:1. Mechi ya pili ilikuwa kati ya Mahakama na Wakili FC ambapo timu hizo
zilitoka suluhu kwa kufungana 1:1, huku goli la Mahakama likifungwa na
Robert Tende.
Mechi ya tatu ilikuwa kati ya TEMESA na Mahakama ambapo Mahakama
iliwazabua TEMESA bao 4:1, magoli ya Mahakama yakifungwa na Kariho Mrisho
(2), goli la tatu likipachikwa na Martin Mpanduzi, kabla ya Chilemba Hassan
kutikisa nyavu kwa kufunga goli la nne.
Mbali na kutangazwa mabingwa katika Bonanza hilo, Mahakama Sports
ilizawadiwa kombe na kutoa mchezaji bora, ambaye ni Kariho Mrisho, Wakili FC
nayo ilipata zawadi ya kombe la mshindi wa pili, huku TEMESA ikiambulia
kutangazwa kama timu yenye nidhamu.
Akizungumza baadaye, Katibu wa Mahakama Sports Taifa Donald Tende
amesema Bonanza hilo liliandaliwa na viongozi wawakilishi wa timu ya Mahakama, Kanda
ya Dar es Salaam, lengo likiwa kuboresha afya na kuimarisha ujirani mwema,
hatua ambayo ni utekelezaji wa nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama katika
kushirikiana na wadau.
Tende, kwa niaba ya uongozi wa Kanda ya Dar es Salaam chini ya
Mwenyekiti wake Jamal Mkumba na Katibu Chilemba Hassan, alisema pia kuwa
wamelichukulia Bonanza hilo kama maandalizi ya Mahakama Sports katika ushiriki
na mashindano ya Mei Mosi yanayotarajiwa kuanza tarehe 14 Aprili, 2023 mkoani
Morogoro.
“Kila Mkoa una uongozi wakilishi ambao uliteuliwa na viongozi
wa Mahakama Sports Taifa ili kusaidiana katika kusimamia michezo na kufanya
mazoezi ili kuboresha afya mahala pakazi. Kwa hiyo kila Mkoa wamekuwa wakifanya
mazoezi na kushiriki mabonanza mbalimbali ya ndani na nje,” amesema.
Mgeni Rasmi katika Bonanza hilo Rajab Mwaliko (juu) akizungumza na wachezaji (chini).
Timu ya Wakili FC.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni