Alhamisi, 16 Machi 2023

KAMATI KATIBA NA SHERIA YASTAAJABISHWA NA UZURI MAJENGO YA MAHAKAMA, YASHAURI YATUNZWE

Na Mary Gwera, Mahakama-Mwanza

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeitaka Mahakama ya Tanzania kuwa na kifungu maalum kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya majengo yake ili yaweze kudumu kwa muda mrefu na kutumika hata kwa vizazi vijavyo.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 16 Machi, 2023 wakati Wajumbe wa Kamati hiyo walipotembelea na kukagua jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC)-Mwanza lililopo Wilaya ya Ilemela Kata ya Buswelu jijini Mwanza.

Akizungumza mara baada ya kukagua jengo hilo, Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Rashid Abdallah Shangazi (Mb) amesema kuwa Mahakama imepiga hatua kubwa katika uboreshaji wa miundombinu ya majengo yake hivyo ni muhimu kuyatunza vyema na kushauri kuwa, Mhimili huo unatakiwa kutengeneza kifungu maalum ambacho kitatengewa fedha zitakazowezesha kufanya ukarabati wa majengo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu.

“Napenda kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuboresha miundombinu ya majengo, hatua ya ujenzi wa miundombinu ya majengo ya Mahakama ni hatua ya juu kwa nchi yetu, kwahiyo ni muhimu majengo hayo kuyatunza ili yaweze kudumu kwa muda mrefu, kuna majengo yaliyotumika enzi za ukoloni lakini yamedumu hadi sasa mfano; Ikulu ya Dar es Salaam, Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na kadhalika, hii ni dhahiri kuwa majengo hayo yametunzwa na kukarabatiwa mara kwa mara na hivyo kuendelea kutoa huduma mpaka sasa,” amesema.

 Kadhalika Mjumbe mwingine wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Ighondo Ramadhani (Mb) amesema kwamba, Tanzania imepiga hatua kubwa katika uimarishaji wa miundombinu na utoaji haki kwa ujumla, hivyo, ameishauri Mahakama kuutangazia umma kuhusu uboreshaji wa huduma mbalimbali unaoendelea kufanyika.

Kwa ujumla Wabunge hao wameridhishwa na jengo hilo na kukiri kuwa limezingatia haki za binadamu kwa makundi yote na kuipongeza Mahakama kwa kuboresha miundombinu.

Akizungumza kwenye kikao kilichofanyika mara baada ya ukaguzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Mwanza, naye Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameishukuru Kamati hiyo na Serikali kwa ujumla kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kuipatia fedha Mahakama za kuendelea na ujenzi na ukarabati wa majengo yake pamoja na kuipa Wizara yake fursa mbalimbali zenye lengo la kuboresha sekta ya sheria kwa ujumla.

“Napenda kuchukua fursa hii, kuishukuru Kamati na Serikali kwa ujumla., na nakiri kuwa, mchakato wa mabadiliko ya utoaji huduma ‘transformation’ mahakamani ni wa kasi kubwa sana, maboresho haya ya Mahakama si tu yanajulikana nchini bali pia hata kwa baadhi ya nchi za wenzetu wanaitaja Mahakama ya Tanzania kama Mahakama ya mfano na iliyopiga hatua katika kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya majengo” ameeleza Mhe. Dkt. Ndumbaro.

Aidha, Waziri ameeleza kuwa, Mahakama inaendelea kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi huku akibainisha kuwa, kwa mwaka huu wa fedha, Mahakama imepanga kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJC) tisa vitakavyojengwa katika mikoa ya Njombe, Simiyu, Ruvuma, Geita, Katavi, Manyara, Singida, Songwe na Lindi.

Akihitimisha kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Florent Laurent Kyombo ameipongeza Mahakama Kanda ya Mwanza kwa jengo zuri na kumtaka Waziri kuwasilisha randama ya bajeti ya Wizara na Mahakama kwa ajili ya maandalizi ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

Awali, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha akitoa taarifa ya jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Mwanza, kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, amesema Mradi huo ulianza tarehe 24 Januari 2020 na kumalizika 28 February 2022 na umetumia kiasi cha fedha za Kitanzania bilioni 8,561,314,505.91 ambapo mpaka sasa Mkandarasi ameshalipwa shilingi 8,133,248,779.75.

“Jengo hili ni miongoni mwa majengo sita (6) yaliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 6 Oktoba, 2021 na dhana ya Vituo jumuishi inalenga kusogeza huduma karibu na wananchi, kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi, kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma za mahakama kwa kuweka huduma za ngazi zote katika jengo moja,” ameeleza Bw. Magacha.

Mtendaji huyo ameongeza kuwa upatikanaji wa Vituo hivyo, umerahisisha pia uendeshaji wa shughuli za Kimahakama kwa kuwa wadau wote muhimu katika mnyororo wa utoaji haki wanapatikana katika jengo moja na vilevile kupunguza gharama kwa wateja wa Mahakama.

Kamati hiyo imehitimisha ziara yake ya kukagua Miradi ya Mahakama, ambapo siku ya kwanza ya ziara yao ilifanyika tarehe 14 Machi, 2023 kwa kukagua Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha ( wa pili kulia) akiwaonesha Wajume wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria sehemu ya Mapokezi ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza wakati walipotembelea Kituo hicho leo tarehe 16 Machi, 2023. Kulia kwa Bw. Magacha ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Florent Laurent Kyombo na wa kwanza kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mhe. Chiganga Tengwa.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha (kulia) akieleza namna Mahakama ya Watoto inavyofanya kazi, Mahakama hiyo ipo ndani ya jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Mwanza. Kulia kwake ni Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mhe. Chiganga Tengwa akifuatiwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro. Wajumbe wa Kamati hiyo wametembelea katika Kituo hicho leo tarehe 16 Machi, 2023.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha akieleza kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria namna Mahakama ya wazi zilivyotengenezwa katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza jambo wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ilipotembelea jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza leo tarehe 16 Machi, 2023.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Bw. Florent Laurent Kyombo akizungumza jambo wakati wa kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika mara baada ya ukaguzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Mwanza.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw.Leonard Magacha (aliyesimama katikati) akiwasilisha mada juu ya jengo la kituo Jumuishi cha Utoaji Haki 'IJC' Mwanza na faida zake.

Makamu mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Florent Laurent Kyombo akieleza jambo wakati wa kikao cha Kamati hiyo iliyotembelea jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Mwanza.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Mlalo, Mhe. Rashid Abdallah Shangazi akichangia jambo mara baada wasilisho la Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ambaye pia  ni Mbunge wa Jimbo la Nyangh'wale, Mhe. Hussein Nassor Amar akichangia jambo wakati Kamati hiyo ilipotembelea jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Mwanza.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge anayewakilisha Wafanyakazi, Mhe. Dkt .Alice Kaijage akichangia jambo wakati kamati hiyo ilipofanya kikao mara baada ya kukagua jengo la 'IJC' Mwanza.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (aliyesimama katikati) akiwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria  na baadhi ya Watumishi wa Mahakama. Wa tatu kushoto aliyesimama mbele ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Bw. Florent Laurent Kyombo.

(Picha na Stephen Kapiga-Mahakama Kuu-Mwanza)

 

 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni