Alhamisi, 16 Machi 2023

KAMATI YA BUNGE YASHAURI UJENZI MAJENGO YA MAHAKAMA UZINGATIE VYUMBA VYA MAMA WANAONYONYESHA

 Na Mwandishi wetu, Mahakama-Mwanza

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria imeshauri Mahakama ya Tanzania kuendelea kutenga chumba cha mama wanaonyonyesha katika miradi ya ujenzi wa miundombinu inayoendelea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 16 Machi, 2023 mjini Mwanza na mmoja wa Wajumbe wa Kamati hiyo Mhe. Dkt. Alice Kaijage wakati wa ziara ya ukaguzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Mwanza.

Amesema mfano walioona leo katika Jengo la Kituo Jumuishi cha UtoajiHhaki cha Mwanza ni vema ramani hiyo ikawa sehemu ya michoro ya Mahakama zote mpya zitakazojengwa hapa nchini kama hatua ya kutambua haki ya mama kunyonyesha mwanae katika mazingira rafiki.

“Niwapongezeni kwa kazi nzuri ya ujenzi wa jengo la kisasa ambalo limethamini wanawake wanaonyonyesha kwa kuwawekea ya  faragha…nashauri ramani za majengo ya Mahakama ambazo mnatarajia kuyajenga ziwe na sehemu ya kunyonyoshea kama tuliyoiona katika jengo hili” amesisitiza.

Katika hatua nyingine Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Rashid Shangazi aliishauri Mahakama na jamii kuhakikisha wanaitunza ili iweze kusaidia katika utoaji haki kwa muda mrefu.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge anayewakilisha wafanyakazi, Mhe. Dkt. Alice Kaijage akichangia jambo wakati Kamati hiyo ilipotembelea jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza. Mhe. Dkt. ameonesha kufurahishwa na uwepo wa chumba maalum cha kunyonyeshea na kushauri majengo mengine ya Mahakama yatakayojengwa yawe na chumba hicho.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni