Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe amewataka Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Mhe. Ngwembe alitoa rai hiyo jana tarehe 15 Machi, 2023 alipokutana na wadau hao muhimu wa Mahakama katika Kanda ya Morogoro ili kuzungumzia masuala mbalimbali ya kiutendaji.
Jaji Mfawidhi huyo aliwasisitiza kutumia lugha nzuri kwa wateja na wananchi kwa ujumla muda wote wanapokuwa katika maeneo ya kazi, kwani kwa kufanya hivyo kutamaliza malalamiko.
“Fanyeni kazi kwa mujibu wa taaluma zenu ili kuondoa malalamiko wakati wa utekelezaji wa amri za Mahakama,” alisema Jaji Ngwembe na kuonya tabia ya baadhi ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama kutumia watu wengine ambao hawajasajiliwa na Mahakama kufanya shughuli hizo.
Amesema hatua zitachukuliwa kwa Dalali ambaye atakiuka utaratibu huo, ikiwemo kufutiwa leseni yake kwani jambo hilo ni kinyume cha kanuni za Madalali, kwa kuzingatia watu hao hawana uelewa wa kutosha kwani hawajapatiwa mafunzo ya udalali.
Sambamba na hilo, Mhe. Ngwembe alionya kama kuna Dalali anajihusisha na vitendo vya kutapeli wateja, maarufu kwa jina na “Kishoka,” kuacha mara moja tabia hizo na kusimamia majukumu yake kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo.
Baada ya kikao hicho,
Jaji Mfawidhi huyo aliwaomba Madalali na Wasambaza Nyaraka hao kwenda katika
eneo linalotumika kutolea elimu ya Sheria Mbashara ndani ya Kituo Jumuishi cha
Utoaji Haki kwa ajili ya kujitambulisha kwa wananchi na kutoa elimu kuhusu kazi
na majukumu yao.
Hatua hiyo ilijitokeza kufuatia baadhi ya wateja kutowatambua Madalali hao wanapotekeleza majukumu yao, ikiwemo kusimamia utekelezaji wa hukumu za Mahakama.
Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama wapo kwa mujibu wa Kanuni za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama za Mwaka 2017 ambao majukumu yao makubwa ni kutekeleza hukumu na amri baada ya Mahakama kusikiliza mashauri na kutoa uamuzi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (aliyekaa wa kwanza kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kikao cha Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama. Kushoto kwa Jaji Ngwembe ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe Augustina Mmbando.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni