Jumatano, 15 Machi 2023

MSAJILI MKUU ATEMBELEA MAHAKAMA YA MWANZO BAGAMOYO

Na Mwandishi wetu-Mahakama ya Tanzania

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amewahimiza watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Bagamoyo kuzingatia na kuyapa kipaumbele maelekezo ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli za kimahakaka kama inavyosisitizwa mara kwa mara na viongozi wa Mahakama.

Mhe. Chuma alitoa wito huo jana tarehe 14 Machi, 2023 alipofanya ziara ya siku moja katika Mahakama hiyo inayoketi Msoga-Lugoba kwa lengo la kujionea namna shughuli za Mahakama zinavyotekelezwa.

Akizungumza na watumishi wa Mahakama hiyo, Msajili Mkuu aliwataka kuwahudumia wananchi kwa viwango vya juu na kuzingatia utoaji wa huduma bora kwa mteja, kwa maana ya customer care.

Mhe. Chuma aliwahimiza kuimarisha tunu ya upendo kati ya mtumishi na mtumishi na hatimaye kuwa na utumishi wenye tija na kufanya kazi kwa weledi, kuzingatia maadili ya kazi na kuwa na uwezo wa kufanya kazi zaidi ya moja.

Kadhalika, Msajili Mkuu huyo alihimiza wasimamizi wa mirathi kufunga mirathi kwa mujibu wa sharia.

Aidha, Mhe. Chuma alielekeza kuwekwa kwa tangazo karibu na barabara kuu linatotambulisha Mahakama ya Msoga-Lugoba ilipo.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akikagua maeneo ya Mahakama ya Mwanzo Bagamoyo katika ziara aliyoifanya jana tarehe 14 Machi, 2023.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akisaini kitabu cha wageni.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (katikati katika picha ya juu na chini) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama hiyo, akiwemo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mhe. Sameera Suleiman (wa pili kushoto).


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni