-Yashauri huduma zitolewazo ziendane na uzuri wa
majengo
Na Tiganya Vincent,
Mahakama -Tabora
Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria leo tarehe 14 Machi, 2023 imekagua Mradi wa Ukarabati
na Upanuzi wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora na kuridhishwa kwa kazi iliyofanyika na kuipongeza Mahakama kwa
utekelezaji mzuri wa Miradi mbalimbali ya uboreshaji wa miundombinu ya majengo
yake.
Akizungumza mara baada
ya ziara ya siku moja ya ukaguzi wa Utekelezaji wa Mradi wa Ukarabati na
Upanuzi wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Makamu Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Florent Laurent
Kyombo amesema kuwa Mahakama ni moja ya Taasisi inayofanya vizuri katika miradi
yake ya ujenzi na hivyo kuwasihi Watumishi wa Mhimili huo kutoa huduma zinazoendana
na uzuri wa miundombinu hiyo.
"Kama Kamati tuna
'oversee' mambo mbalimbali yanayofanyika Serikalini, hivyo napenda kuchukua
nafasi hii kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa uboreshaji wa huduma mbalimbali
unaoendelea ikiwa ni pamoja na maboresho ya miundombinu ya majengo, kwakweli
mnaupiga mwingi," amesema Mhe. Kyombo.
Mhe. Kyombo ameishukuru
Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa Mahakama ya Tanzania kwa ajili ya
uboreshaji wa miundombinu ya utoaji haki kwa wananchi.
Naye, Mbunge wa Jimbo
la Kiteto ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Edward Ole Lekaita
amesema ubora wa majengo ya Mahakama unaridhisha na kuongeza Mahakama
imeitendea haki fedha waliyopewa na Serikali kwa ajili ya shughuli hiyo ya
ukarabati.
Amesema uboreshaji na
ukarabati wa Mahakama hiyo umewawezesha Maafisa wa Mahakama na Wadau wao
kutekeleza majukumu yao ya utoaji wa haki kwa wananchi katika mazingira mazuri.
Kwa upande wake, Mbunge
wa Viti Maalum, Mhe. Khadija Shaaban almaarufu Keysha amesema Mahakama
imeitendea haki fedha za ukarabati walizopatiwa na Serikali na kushauri kuweka
'Lift' maalum kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum.
Awali, Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Mradi huo umetumia
kiasi cha fedha za Kitanzania bilioni 2.5 na ulianza kutekelezwa mwezi Juni
mwaka 2021 na kukamilika Septemba, 2022.
Amesema kuwa, hadi sasa
Mkandarasi ameshalipwa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 ambayo ni sawa ya
asilimia 61 na bado anadai milioni 900 ambazo wanaendelea kushughulikia.
Prof. Ole Gabriel,
ameongeza kuwa, kukamilika kwa mradi huo kumesaidia kuboresha mazingira ya
utendaji kazi kwa watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na kuahidi kuwa
watahakikisha kuwa haki inapatikana kwa ubora.
Aidha Mtendaji huyo
amewataka Wajumbe wa Kamati hiyo kuisaidia Mahakama kwa kuwaeleza wananchi
kuhusu uboreshaji wa huduma mbalimbali za Mahakama unaoendelea ikiwemo matumizi
ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wakati ufunguaji wa mashauri na
usikilizaji wa mashauri.
Kamati hiyo inatarajia pia kutembelea jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC)-Mwanza tarehe 16 Machi, 2023.
Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwakaribisha Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria pindi walipotembelea Mradi wa Ukarabati na upanuzi wa Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Tabora leo tarehe 14 Machi, 2023. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Florent Laurent Kyombo (Mb).
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha (kushoto) akiwaonesha Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kibao cha uzinduzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora pamoja na kuelezea historia jengo hilo ambalo awali lilikuwa likitumika kama Ofisi ya Serikali za Mitaa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Amour Khamis akizungumza jambo na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Florent Laurent Kyombo (hayupo katika picha) wakati Makamu Mwenyekiti huyo na baadhi ya Wajumbe alioambatana nao walipomtembelea Jaji Mfawidhi ofisini kwake Mahakama Kuu-Tabora.
Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza jambo alipokuwa ofisini kwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Paulina Gekul akizungumza jambo wakati yeye pamoja sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria walipokuwa ofisini kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Amour Khamis (hayupo katika picha).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Amour Khamis akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya ujumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, wa tatu kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Florent Laurent Kyombo (Mb). Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Paulina Gekul, wa pili kushoto ni Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, wa tatu kushoto ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Rashid Abdallah Shangazi (Mb), wa kwanza kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Dkt. John Rogath Mboya na wa kwanza kulia ni Mtendaji-Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Bw. Ginaweda Nashon.
Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasilisha taarifa ya Ukarabati na Upanuzi wa jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria walipotembelea Mradi huo mapema leo kwa ajili ya ukaguzi.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria, Watumishi wa Mahakama na wageni waalikwa wakifuatilia kwa umakini wasilisho lililokuwa likitolewa na Mtandaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo katika picha).
Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Utawala, Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Florent Laurent Kyombo (Mb) akizungumza jambo baada la wasilisho lililotolewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama. Mwenyekiti huyo amepongeza kazi nzuri ya ukarabati na upanuzi wa jengo wa Mahakama Kuu Tabora ulivyofanyika. Kulia ni Katibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Bw. Frank Nkya.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Edward Ole Lekaita (Mb), akipongeza kazi nzuri ya ukarabati na upanuzi wa jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni