Na Faustine Kapama – Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 13 Machi, 2023 amemkabidhi Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Mhe. Charles Mnzava nyenzo
za kufanyia kazi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.
Tukio hilo ambalo
lilishuhudiwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher
Siyani, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma pamoja na
viongozi wengine wa Mahakama limefanyika katika Ofisi ya Jaji Mkuu katika jengo
la Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam.
Akitoa nasaha na
maelekezo baada ya tukio hilo, Jaji Kiongozi alimpongeza Mhe. Mnzava kwa kuaminiwa
na kuteuliwa kushika wadhifa huo. Alimkumbusha mambo matatu muhimu ambayo
anatakiwa kuyazingatia anapotekeleza majukumu yake.
Mhe. Siyani amemhimiza Hakimu
Mfawidhi huyo kusimamia maadili ya Mahakimu na watumishi wa kada nyingine katika
Mkoa wake na kuwaunganisha wote ili waweze kutimiza majukumu yao vizuri, hatua
itakayomwezesha kupata matokeo.
“Unaposimamia kazi ya
msingi ya Mahakama ya kusikiliza na kuamua mashauri lazima kila mtumishi anakuwa
mwadilifu. Jamii haitatuamini tukiwa na watumishi wasiowaadilifu hata tunapotoa
hukumu zilizosahihi. Kazi yetu ni ya imani ambayo wale tunaowahudumia lazima
wawe na imani na sisi,” alieleza.
Hata hivyo, Jaji Kiongozi
alimweleza Hakimu Mfawidhi huyo kuwa ili aweze kusimamia maadili lazima aanze yeye
mwenyewe kama kiongozi kuwa mwadilifu ndiyo aweze kusimamia wengine, kwani akiyumba
atayumbisha jahazi.
“Hatua uliyoifikia leo ni
kubwa, ambayo itapunguza uhuru uliokuwa nao, itakunyima fursa ya kufanya
mengine ambayo ulikuwa unayafanya kwa uhuru kwa sababu watu watakutazama kwa
jicho jingine,” Mhe. Siyani alisema.
Jaji Kiongozi alieleza
kuwa anaitazama Mtwara kama Kanda ambayo inahitaji kiongozi ambaye ataunganisha
watumishi. Amesema ufuatiliaji ambao umekuwa ukifanyika kwa miaka miwili
iliyopita umeonyesha uwepo wa changamoto ya makundi.
“Ili ufanikiwe lazima
ufanye kila linalowezekana kuhakikisha una watumishi wa taasisi moja ambayo ni
Mahakama ya Tanzania. Ukiyaendeleza na wewe ukawa na kundi la kwako,
hautafanikiwa. Kupanda ni jambo gumu, lakini kuanguka ni jambo rahisi.
Usikubali kuangushwa,” alisema.
Kadhalika, Mhe. Siyani
alimtaka Hakimu Mfawidhi huyo kusimamia majukumu ambayo amepewa, ikiwemo majukumu
ya kimahakama yanayohusisha, pamoja na mambo mengine, kusikiliza mashauri na majukumu
ya usimamizi na ukaguzi.
“Usiwe Mfawidhi ukaacha
kusikiliza mashauri na unaposikiliza mashauri simamia sana kuhusu matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Wewe mwenyewe uwe mfano kwa sababu huko
ndiko tunakoelekea, tusisikilize mashauli kizamani,” alisisitiza.
Jaji Kiongozi amemtaka pia
kama Hakimu Mfawidhi kuimarisha, kuwa mbunifu na kuonyesha tofauti kati ya Mkoa
wake na Mkoa mwingine kwenye matumizi ya TEHAMA kwa sababu hakuna njia ya
kurudi nyuma.
Awali, akimkaribisha Jaji
Mkuu kukabidhi nyenzo hizo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert
Chuma alieleza kuwa Mhe. Mnzava aliajiliwa mwaka 2005 na kufanya kazi katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kabla ya
kuhamishiwa katika Baraza la Ardhi na Nyumba mwaka 2008.
Ameeleza kuwa mwaka 2020,
Mhe. Mnzava alihamia katika Mahakama ya Wilaya Tarime hadi mwezi Mei 2021
alipoteuliwa kuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Nanyumbu na amehudumu
katika Mahakama hiyo hadi Februari 2023 alipoteuliwa kuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama
ya Hakimu Mkazi Mtwara.
Viongozi wengine
waliohudhuria hafla hiyo fupi ni Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Silvester
Kainda, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Hussein Mushi na Mtendaji kutoka
Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Bi Maria Itala.
Viongozi kadhaa waliohudhuria hafla hiyo. Kutoka kulia ni Naibu Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi, Mtendaji kutoka Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Bi Maria Itala, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Hussein Mushi na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Mhe. Charles Mnzava.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Mhe. Charles Mnzava akifuatilia kwa makini yaliyokuwa yanajiri kwenye hafla ya kukabidhiwa nyenzo za kufanyia kazi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimpongeza Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Mhe. Charles Mnzava baada ya kumkabidhi nyenzo za kufanyia kazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni