Jumamosi, 11 Machi 2023

TUMIENI MAFUNZO MLIYOPATA KUTIBU CHANGAMOTO: JAJI MALATA

Na. Evelina Odemba-Mahakama, Morogoro.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Gabriel Malata amewahimiza wahitimu wa mafunzo ya Haki Jinai awamu ya pili kutumia elimu waliyopata kutatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili katika kutekeleza majukumu yao. 

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo jana tarehe 10 Machi, 2023, Mhe. Malata alisema kuwa ni imani yake zile changamoto zilizokuwa zikiwakabili na kusababisha utoaji haki kuchelewa zimepatiwa mwarobaini baada ya washiriki wote kupatiwa elimu ambayo itaonekana katika uwajibikaji. 

“Tusichoke kujifunza kila iitwapo leo, kila mmoja katika nafasi yake ajitathimini kwa kazi anayoifanya, wote tuna kusudi la kutoa huduma bora kwa mwananchi,” alisema. 

Mhe. Malata aliomba upande wa Mawakili wa Serikali kuendelea kutoa ushirikiano kwa wapelelezi ili wote wawe na kasi moja ya utoaji haki kwa wakati. 

Naye mshiriki wa mafunzo, Bw. Deogratius Chami alitoa shukurani kwa watoa mada na waandaaji kwa kuwajengea uwezo mpana katika ufanyaji kazi mara watakaporejea kwenye vituo vyao. 

“Ukweli tumetoka na fikra tofauti kabisa na tulivyokuja,” alipongeza Bw. Deogratius na kuomba mafunzo hayo kuwafikia wadau wote katika taasisi za Haki Jinai ili kuwe na mtazamo mmoja wakati wa utekelezaji wa majukumu yao. 

Mafunzo ya Haki Jinai awamu ya pili yalifunguliwa mnamo tarehe 6 Machi, 2023 yakijumuisha washiriki 62 ambao wametunukiwa vyeti. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuendelea kwa awamu nyingine, lengo ni kuwafikia washiriki 250 wanaotoka katika taasisi ambazo ni wadau wa Haki Jinai.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Gabriel Malata akiongea na washiriki wa mafunzo ya hiki jinai (hawapo pichani) wakati wa kufunga mafunzo awamu ya pili.
Sehemu ya wanafunzi (juu na chini) ikifuatilia hotuba ya kufunga mafunzo hayo kutoka kwa mgeni rasmi, Jaji Gabriel Malata (hayupo pichani).

Meza Kuu ikipokea maoni ya watoa mada. Katikati ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Gabriel Malata, kulia kwake ni Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Arnold Kirekiano na kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe Livin Lyakinana.
Washiriki (juu na chini) wakitunukiwa vyeti na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Gabriel Malata wakati wa kuhitimu mafunzo hayo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni