·Afisa TEHAMA auchambua namna unavyofanya kazi
Na
Faustine Kapama`– Mahakama, Morogoro
Mfumo wa Sema na Mahakama
ambao ni mpya wa kielekroniki (e-complaint) wa kutoa na
kupokea maoni, maulizo na malalamiko au mrejesho kutoka kwa wananchi
umekamilika
na upo tayari kuanza kutumika.
Hayo yamebainishwa na afisa
kutoka Kurugenzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bw. Lazaro
Sanga alipokuwa anawasilisha mada kuhusu mfumo huo unavyofanya kazi kwenye mafunzo
yanayofanyika mjini hapa yakijumuisha maafisa wenzake waliotoka Kanda zote za
Mahakama ya Tanzania.
“Mfumo huu umekamilika
kwa asilimia 98 na unaweza kuanza kutumika. Tayari baadhi ya viongozi wameanza
kupokea ujumbe mfupi kutoka kwa wananchi. Mfumo huu haujajengwa kwa ajili ya
kupokea malalamiko pekee, bali pia mwananchi ana uhuru wa kutoa maoni, mrejesho,
mapendekezo au pongezi,”alisema.
Amewaambia maafisa TEHAMA
wenzake wanaoshiriki mafunzo hayo, ambayo yameingia siku ya nne, kuwa ili
mwananchi aweze kutuma lalamiko, pendekezo au maulizo anatakiwa kuwa na simu ya
mkononi (smartphone), kompyuta au kishikwambi (tablet).
Bw. Sanga alieleza kuwa mfumo
huo unamwezesha mwananchi kutuma lalamiko wakati wowote na mahali popote ila tu
anatakiwa kuwa na mtandao mzuri na humwezesha kutuma lalamiko lake kwa njia ya
msimbo kwa kubonyeza *152*00#.
“Mfumo unaruhusu
mwananchi kufungua akaunti ya Sema na Mahakama, anachotakiwa ni kujaza taarifa
zake kwa usahihi ili aweze kupata mrejesho wa pale anapotuma lalamiko lake. Mfumo pia unatoa nafasi ya kutuma lalamiko bila
kujulika. Ili uweze kupata mfumo anatakiwa kubonyeza https://sema.judiciary.go.tz,”
alieleza.
Alitaja njia mbili ambazo
zinaweza kutumiwa na mwananchi kujua lalamiko lake kama limepokelewa na
kujibiwa au la. Njia hizo ni kwa kutumiwa ujumbe mfupi kupitia simu yake ya
mkononi endapo alitumia akaunti yake ya Sema na Mahakama au alijaza taarifa zake
pia kwa kutumia namba ya kitambulisho ya lalamiko kupitia tovuti ya Sema na Mahakama,
Mobile App au Msimbo.
Kwa
mujibu wa Afisa TEHAMA huyo, mfumo umegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni
sehemu ya wananchi kutuma
malalamiko bila kujulikana, kutuma malalamiko kwa kuweka taarifa na kwa
kufungua akaunti. Amesema sehemu ya pili ni kwa watumishi wanayoitumia kujibu
malalamiko na mapendekezo ya wananchi.
Jana
jioni tarehe 8 Machi, 2023, washiriki hao wa mafunzo walipitishwa kwenye mada
inayohusu mabadiliko na jinsi ya kutawala mabadiliko yanayotokea ndani na nje ya
mtu. Mada hiyo iliwasilishwa na Mhadhiri huru wa Vyuo vya Mafunzo ya Utawala
Afrika Mashariki na Kusini, ambaye pia ni Mshauri Mtaalam Binafsi, Dkt. Endrew
Msami.
Akiwasilisha
mada hiyo, Dkt. Msami aliwashauri maafisa TEHAMA hao kwenda na mabadiliko
kulingana na Mahakama ya Tanzania ilivyobadilika, kwani kwa kufanya hivyo wataweza
kufanikisha malengo ya taasisi wanayoitumikia, hivyo kutoa huduma bora kwa jamii
inayowazunguka.
“Anzeni
kutengeneza mabadiliko ndani yenu ili mabadiliko ya nje yaweze kuleta matunda
mazuri kupitia utendaji wenu wa kazi. Badilikeni ili muendelee kuwa watu bora
kila siku, unapobadilika ili iwe mtu bora leo unatakiwa na kesho ubadilike ili uendelee
kuwa mtu bora kesho kutwa,” alieleza.
Amewakumbusha
washiriki hao wa mafunzo kuwa Mahakama ya Tanzania siyo ya jana kutokana na
mabadiliko makubwa ambayo imeyafanya katika kuhakikisha jukumu lake kuu la
utoaji haki linaendelea kutekelezwa kwa ufanisi unaotakiwa, hivyo na wao
wanatakiwa kwenda na mabadiliko hayo ili wasiachwe nyuma.
Afisa kutoka Kurugenzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bw. Lazaro Sanga akieleza jinsi mfumo huo unavyofanya kazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni