Na Eva Leshange, Mahakama Singida
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi
wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Mkoa wa Singida, Dkt. Athumani Bunto jana tarehe
14 Aprili, 2023 alitembelea wanachama wa TUGHE wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Singida na kuwapa habari njema kuhusu fedha zinazokatwa kwenye mishahara yao.
Dkt. Bunto ambaye aliambatana na Katibu Msaidizi wa TUGHE, Bi Hadija Kapiligi aliwaeleza watumishi kuwa kwa sasa fedha zao walizokuwa wanakatwa zimeshaanza kuingizwa kwenye akaunti za matawi.
“Fedha zilizokuwa
zinakatwa zimeanza kuingizwa kwenye akaunti za matawi, hivyo viongozi wa tawi
hili hakikisheni akaunti inafunguliwa. Fedha hizi zitasaidia kuendesha shughuli
mbalimbali za tawi, ikiwemo kuendesha vikao vya TUGHE na kufanya malipo
mbalimbali,” alisema.
Aliwasisitiza watumishi
kuendelea kujiunga na vyama vya wafanyakazi kwani vipo kisheria na vimekuwa na faida
nyingi, ikiwemo kutetea maslahi yao na kuwa mdhamini wa mwanachama anapokuwa na
mashauri ya kinidhamu.
“Vile vile vyama hivi vya
wafanyakazi vinasaidia kuunganisha watumishi wote wa juu, wa kati na wa chini” Mwenyekiti
huyo aliwaambia watumishi hao wa Mahakama katika ziara yake ya pili kutembelea
tawi hilo.
Dkt. Bunto alisisitiza
Dunia inapoelekea kuadhimisha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi na kwakuwa
kutakuwa na uchaguzi wa kutafuta wafanyakazi hodari ni vyema kuzingatia
kuchagua watumishi wenye sifa.
Akizungumza katika tukio
hilo, Katibu Msaidizi wa TUGHE alibainisha sifa hizo, ikiwemo kuwa mwanachama
wa TUGHE, anayetimiza wajibu wake kazini, anayependa na kuthamini kazi, hodari
na jasiri na mwenye kusikiliza ushauri wa wengine.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama wakisikiliza kwa makini.
(Habari hii
imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mwanza)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni