Na Magreth Kinabo, Mahakama Mkuranga
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amewataka watumishi wa kanda hiyo kutoa huduma ya utoaji haki kwa viwango bora ili kuhakikisha jukumu hilo linatelelezwa ipasavyo na kwa wakati.
Akizungumza leo tarehe 28 Aprili 2023 wakati akifunga kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa kanda hiyo lililofanyika Mkuranga mkoani pwani, alisema kila mtumishi ana wajibu wa kutoa huduma inayoridhisha na yenye viwango bora.
“Unapotoa huduma ya utoaji haki unapaswa kujiuliza kuwa imekidhi viwango bora vinavyotakiwa, hivyo kila mtumishi anaowajibu wa kuboresha utendaji wake wa kazi ili kuweza kutimiza jukumu hilo la msingi,” alisema Jaji Salma.
Jaji Salma aliongeza kwamba watumishi hao, wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano kwa kuwa kufanya hivyo kunasaidia kubadilishana mawazo na uzoefu wa kazi kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwenye utendaji wao wa kazi huku akisema milango ya ofisi yake iko wazi kwa mtumishi yoyote yule ili kuhakikisha gurudumu lla utoaji haki linasongambele.
Aliongeza kuwa watumishi hao, wanowajibu wa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma zao.
Aliwataka watendaji wa mahakama zilizopo katika kanda hiyo, kuhakikisha bajeti wanayoipata inazingatia maslahi ya watumishi wa ngazi za chini.
“ Tuwe waangalifu kwa chochote tunachokipata tugawane ili wote tuweze kula kwenye sahani moja,” alisisitiza.
Kwa upande wake Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Sundi Fimbo akitoa takwimun za usikilizaji wa mashauri kuanzia Januari 2022 hadi Aprili 25 2023 zinaonesha kuwa bado kuna changamoto za mlundikano wa mashauri kwa zaizi ya asilimia 100.
Alizitaja mahakama zenye mlundikano huo kuwa ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu yenye mlundikano wa mashauri 406, Mahakama Kuu mashauri 249, Mahakama ya Wilaya ya Ilala nashauri 148 na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni mashauri 145.
Alizitaja changamoto za mlundikano huo ni kuwa ni kutokamilika kwa upelelezi kwa wakati, mzigo mkubwa kwa majaji hasa Mahakama Kuu na kutokuwa na mpango ‘Case Management’.
Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Edward Mbara alisema hadi kufikia tarehe 31 Machi 2023 kanda hiyo inawatumishi 632 kati ya hao, mahakimu 166 na 466 kada nyingine.
Alisema kanda hiyo ina upungufu wa vitendea kazi kama vile kompyuta, uchakavu wa samani za ofisi na magari.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni