- Wananchi wapongeza usikilizwaji wa mashauri mtandao
Na Aidan Robert, Mahakama Kuu Kigoma
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Kanda imejipanga kuvuka lengo la kusikiliza Mashauri 826 kwa njia ya mtandao ikiwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za Mahakama nchini za kutoa huduma zake kwa njia ya mtandao.
Hatua hii imedhihirishwa kwa vitendo tarehe 27 Aprili, 2023 ambapo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha alisikiliza mashauri yote yaliyopangwa akiwa ofisini kwake huku wahusika wa mashauri husika wakiwa katika chumba maalum cha Mkutano mtandao ‘Video Conference’, kilichopo Mahakama Kuu Kigoma na maeneo mengine ikiwa ni njia ya kuwafundisha wananchi na wadau kuzoea maboresho hayo.
Mhe. Mlacha alisema kuwa, kitendo hicho kinafanyika wakati ambapo Mahakama Kanda ya Kigoma imedhamiria kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao na kuutumia njia ya kutoa elimu wakati mashauri yakiwa yanasikilizwa.
“Mpaka sasa, kati ya Januari hadi Machi 31, mwaka huu, Kanda ya Kigoma imesikiliza mashauri 353 kwa njia ya mtando (Video Conference),” alisema Mhe. Mlacha.
Aidha, Jaji Mfawidhi huyo alisema kwamba, elimu kwa umma inatolewa pia kupitia vipindi vya redio Joy ya mkoani humo ambavyo hurushwa kila ijumaa ya kwanza na ya mwisho kwa kila mwezi.
Jitihada hizo za usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya mtandao zimeungwa mkono pia na Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Mkoa wa Kigoma, Bw. Arnold Simeo ambaye ameipongeza Mahakama kwa hatua hii kubwa ya matumizi ya TEHAMA na kwa kuimarisha vifaa vya usikilizaji wa mashauri hayo kwa ajili wadau wa Mahakama hatua ambayo anaeleza kuwa itasaidia kupunguza wingi wa mashauri mahakamani.
“Njia hii inapunguza gharama za kusafiri kuja mahakamani hata kwa shauri la kutajwa,” kama ambavyo wananchi wakibainisha huku Bi. Husina Masood akieleza kuwa ataenda kuwa shuhuda wa maboresho makubwa ya Mahakama Kanda ya Kigoma ambapo alishangazwa kuona shauri lake likisikilizwa bila kuonana moja kwa moja na Jaji kwenye chumba cha Mahakama.
Kwa upande wake Bw. Double Petro Bujiji, Mkazi wa Kasulu alieleza kwamba, katika shauri lao ambalo kwa siku ya kwanza leo lilisikilizwa kwa njia ya ‘Video Conference’ ambapo Jaji Mlacha aliwasikiliza kwa njia hiyo. “Naipongeza Mahakama kwa hatua hii, Mahakama itawapunguzia sana gharama ya usafiri kutoka Kasulu mpaka kuja kigoma kufuata huduma za Mahakama Kuu,” alisisitiza Bw. Bujiji.
Aidha katika moja ya mashauri yaliyopangwa siku hiyo, Wakili wa Kujitegemea, Bw. Thomas Msasa alishiriki katika moja ya shauri yaliyosikilizwa mbele ya Mhe. Lameck Michael Mlacha, ambapo alisema, “naipongeza Mahakama kwa kutenga chumba maalum na uwepo wa vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya video conference katika jengo hili imetusaidia Mawakili kutumia na wateja wetu kusikiliza mashauri mengi tunayoyasimamia bila kuwa na changamoto ya mtandao.”
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha akiwahudumia wananchi ofisini kwa kusikiliza mashauri yao kwa njia ya Tehama (video conference) akiwa ofisini kwake.
Wakili kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bw.Arnold Simeo (kushoto) akiwa na wananchi waliokuwa na mashauri yao siku hiyo katika chumba maalum cha huduma ya 'video conference' kilichopo katika jengo la Mahakama Kuu Kigoma.
Wakili wa Kujitegemea mkoani Kigoma, Bw. Thomas Msasa akiwa tayari kuingia chumba maalum cha 'video conference' ili kusikiliza shauri analolisimamia lililopo mbele ya Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha.
Sehemu ya wananchi waliofika kusikiliza mashauri yao kwa njia ya mtandao (video conference) Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma. na mashauri, Kulia ni Bi. Husina Masudi na kushoto ni Bw. Double Petro Bujiji.
Picha ya pamoja ya wananchi waliokuwa wakisubiri huduma ya Mahakama kuanza katika chumba maalum cha 'Video Conference' katika kesi husika ili kufuatilia usikilizwaji wa mashauri yao, mbele ya Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Lameck Mlacha.
(Imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni