Jumamosi, 29 Aprili 2023

MSAJILI MKUU WA MAHAKAMA ATEMBELEA MAHAKAMA KUU MANYARA

Na Christopher Msagati-Mahakama, Manyara

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma jana tarehe 28 Aprili, 2023 alitembelea Mahakama Kuu Manyara na kupongeza juhudi zinazofanywa na watumishi katika kupunguza mlundikano wa mashauri.

Mara baada ya kuwasili mahakamani hapo, Mhe. Chuma alipokelewa na wenyeji wake, akiwemo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza pamoja na viongozi wengine.

Wengine waliokuwepo kwenye mapokezi hayo ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Bernard Mpepo, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda, Bw. Jacob Swalle pamoja na watumishi wengine ya Mahakama.

Katika ziara hiyo, Msajili Mkuu alipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Mahakama, ikiwemo takwimu za mashauri kutoka ngazi zote za Mahakama zilizopo katika Kanda hiyo.

Katika taarifa hiyo, Mhe. Mpepo alimweleza Msajili Mkuu uwepo wa changamoto ya ufinyu wa bajeti, hususan tangu kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara mwezi Novemba 2022.

Mhe. Chuma pia alipokea changamoto mbalimbali kutoka kwa watumishi, ikiwemo upandishwaji vyeo, miundombinu ya majengo isiyoridhisha, hususan katika Wilaya za Hanang’ na Simanjiro.

Katika kujibu hoja hizo, Msajili Mkuu aliwaomba watumishi hao kuwa na subira wakati changamoto zao zinafanyiwa kazi katika ngazi ya Mahakama Kuu. Alisema changamoto hizo walizozitoa zipo nchi nzima na zilishafika Makao Makuu na kwa sasa zinashughulikiwa.

Wakati huo huo, watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara jana tarehe 28 Aprili, 2023 walifanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi, ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika tangu kuanzishwa kwa Kanda hiyo.

Katika kikao hicho, watumishi walipata elimu kuhusu uundwaji wa Mabaraza ya Wafanyakazi kutoka kwa Afisa Kazi Mkoa wa Manyara Bw. Deodatus Munishi kwa vile Kanda hiyo ya Mahakama ni mpya.

Vile vile, watumishi hao walifanya uchanguzi wa viongozi wa Baraza katika ngazi mbalimbali, zoezi lililosimamiwa na Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Manyara, Bw. Honest Temba na Bw. Munishi.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akisalimiana na baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara alipowasili mahakamani hapo jana tarehe 28 Aprili, 2023.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Bernard Mpepo akisoma taarifa ya utekelezaji kwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (aliyesimama) akiongea na watumishi (picha chini).

Watumishi wa Mahakama wakimsikiliza Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (wa pili kushoto waliokaa), viongozi wengine na watumishi wa Mahakama Kuu Manyara.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni