Na Mayanga Someke-Mahakama, Sumbawanga
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Sumbawanga,
Mhe. Amir Mruma jana tarehe
28 April, 2023 aliongoza kikao cha Baraza la
Wafanyakazi wa Kanda hiyo, kujadili
mambo mbalimbali yanayohusu wafanyakazi wa Mahakama kutoka Mikoa ya Katavi na
Rukwa.
Kadhalika, kikao hicho kililenga
kuangalia hoja za
wafanyakazi na maazimio kuelekea Baraza Kuu la Wafanyakazi Taifa. Mhe. Mruma
aliwaambia wajumbe kuwa Mabaraza hayo yanaundwa kwa mujibu wa sheria na kwa
kufuata misingi halali.
‘’Hoja za
wafanyakazi zijadiliwe na kutolewa majibu yake na wafanyakazi wapate mrejesho
kupitia Baraza hili na tufanye maazimio kwa pamoja ili tuwe na kauli moja sisi
sote kama wafanyakazi,’’alisema Mhe. Mruma alipokuwa anafungua kikao hicho.
Jaji Mfawidhi alipendekeza kuwa watumishi wasio
maofisa wa Mahakama (Non-Judicial Officers) wapate sare itakayoendana na
maadili ya Mahakama, hivyo mwaka wa fedha 2023/2024 itengwe bajeti kwa ajili ya
kuwanunulia watumishi hao, hasa wale wanaoingia mahakamani ili kuwa na sare
itakayowatambulisha kwa wateja.
“Nasisitiza tutenge bajeti kwa ajili ya sare kwa
watumishi wanaongia mahakamani na pia tusimame imara kuzungumzia mazuri ya Mhimili
wetu wa Mahakama kuanzia Mhudumu mpaka nafasi ya Jaji na sio kuiongelea
Mahakama kama idara,’’aliongeza.
Jaji Mfawidhi aliwashukuru wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi
na kuwaahidi kuendeleza ushirikiano na TUGHE ili kuweka uwiano was pale panapotokea
jambo linalowahusu wafanyakazi.
Baada ya ufunguzi wa kikao, Katibu wa TUGHE, Bw. Ayub Nyarobi alianza kusoma agenda mbalimbali za kikao ambapo kwa kauli moja walizipitisha bila mabadiliko na kumalizia kusoma muhtasari wa kikao cha Baraza kilichopita.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Amir Mruma akizungumza wakati anafungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi.
Viongozi wa Mahakama Kanda ya Sumbawanga wakifuatilia ufunguzi wa kikao hicho. Kuanzia kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Bw.
Emmanuel Munda, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Maira Kasonde, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe, Gway
Sumayi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga, Mhe. Kisasila Malangwa.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Sumabwanga kutoka Mikoa ya Katavi na Rukwa wakiwa kwenye kikao hicho.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni