·Timu za Mpira wa Miguu, Kamba na Riadha zachomoza
Na
Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Timu ya mpira wa miguu na
timu ya kamba wanaume toka Mahakama Sports Klabu zimeibuka mshindi wa nne
katika mashindano ya kuwania kombe la Mei Mosi yanayoendelea mkoani hapa.
Michezo hiyo ilifanyika
jana tarehe 28 Aprili, 2023 katika uwanja wa Jamhuri ambapo kwa upande wa mpira
wa miguu Mahakama ilicheza na Tanesco na kupata goli moja (1) huku Tanesco
ikiondoka na goli mbili (2) na kwa upande wa Kamba, Mahakama ilivutana na Ikulu.
Michezo hii yote
ilishuhudiwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel ambaye alitoa pongezi zake za dhati kwa washiriki wote na kusema kuwa
hakika wamefanya kazi nzuri na wameiwakilisha vyema Mahakama ya Tanzania upande
wa michezo na hata katika nidhamu.
Mara baada ya michezo
kumalizika Mtendaji Mkuu alipata wasaa wa kuzungumza na wachezaji wote
wanaoiwakilisha Mahakama katika mashindano hayo. Alisema alifika kuwaunga mkono
kwa niaba ya uongozi wa juu wa Mahakama ukiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Alisisitiza kuwa katika michezo
kuna vingi vya kujifunza zaidi ya kuwa washindi pekee, kwani kupitia mchezo huo
alioushuhudia ameona vipaji vingi na kazi kubwa ambayo wanamichezo hao
wameifanya uwanjani.
Prof. Ole Gabriel aliwataka
wanamichezo hao kutokata tamaa kwa kuwa hawakufanikiwa kupata nafasi ya kwanza
kama walivyokusudia. “Nilitaka kuondoka ila nikaona nisubiri kwani mtu
asiposhinda ndio anahitaji kutiwa moyo zaidi kuliko hata angeshinda, kikubwa nawaomba
kutokata tamaa, mimi Mtendaji Mkuu wa Mahakama sijakata tamaa sasa nyie
mtakataje tamaa?” aliuliza.
Sambamba na hilo,
Mtendaji Mkuu alivutiwa na namna michezo ilivyoweka ushirikiano baina ya kada
tofauti tofauti ndani ya Mhimili wa Mahakama na kueleza, “Nimeona Hakimu
anafunga magoli na anapasiwa mpira na RMA, golikipa nae ni Hakimu ni jambo zuri,
naamini mashindano yajayo tutafanya vizuri zaidi,” alisema. Alimwomba Kocha Spear
Mbwembe asikate tamaa na kuahidi kuwa watajitahidi kuboresha kwa kuwezesha
wanamichezo kupata wasaa mzuri wa kukaa kambini kwa mazoezi na hata kuwezesha
wanamichezo wengi kushiriki kadri ambavyo bajeti itaruhusu.
Awali, kabla ya kuanza
kwa mechi hizo za kuwania mshindi wa nne, wanamichezo wa Mahakama walipata
fulsa ya kutembelewa na Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali Watu, Bi. Beatrice
Patric katika kambi waliyofikia na kuzungumza nao machache. Bi. Patrick aliwaambia
wanamichezo hao kuwa michezo inajenga urafiki na kuleta umoja na afya, hivyo hatua
waliyofikia ni nzuri na Mahakama iko pamoja nao.
Naye Mwenyekiti wa
Mahakama Sports Klabu Wilson Dede alihitimisha kwa kusema kuwa mwisho wa
mashindano haya ndio mwanzo wa kujipanga kwa ajili ya michezo ijayo.
Alieleza kuwa wao kama
viongozi wamepanga kukaa kikao kujadili kama wanamichezo ili kuboresha katika mashindano
yajayo waweze kufanya vizuri zaidi.
Mashindano ya kuwania
kombe la mei mosi yanategemewa kumalizika leo tarehe 29 Aprili, 2023. Katika
michezo mingine, Mahakama imeibuka mshindi wa pili kwenye bao, mshindi wa nne
karata na mshindi wa nne riadha.
Kumalizika kwa mashindano haya ni mwanzo wa maandalizi ya michezo inayofuata ya SHIMIWI ambayo inatarajiwa kufanyika mkoani Iringa kwa mwaka wa 2023.
Kikosi cha timu ya Kamba
(ME) toka Mahakama kikivutana na Kamba (ME) toka Ikulu (hawapo pichani) huku
wakishuhudiwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel (aliyevaa traki suti ya bluu).
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyevaa nguo ya bluu)
akiwasili katika uwanja wa Jamuhuri Morogoro na kupokelewa na Mkurugenzi
Msaidizi wa Utawala Stephen Magoha na Mwenyekiti wa Mahakama Sports Klabu
Wilson Dede (aliyempa mkono) ili kushuhudia timu za Mahakama zilizokuwa
zinacheza kuwania mshindi wa nne.
Timu ya mpira wa miguu
toka Mahakama Sports Klabu wakiwa katika picha ya pamoja na kocha wao Spear
Mbwembe.
Mkurugenzi Utawala na Raslimali
Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patric akiwa katika picha ya pamoja
na wachezaji wa timu ya mpira wa pete toka Mahakama Sports Klabu.
Mkurugenzi wa Utawala na
Raslimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patric akiwa katika picha ya
pamoja na viongozi wa Mahakama Sports Klabu alipotembelea kambi ya wanamichezo
hao mkoani Morogoro.
Mkurugenzi Msaidizi wa
Utawala Stephen Magoha akisalimiana na kikosi cha timu ya mpira wa miguu toka
Mahakama sports klabu kabla ya kuanza kwa mechi dhidi ya Tanesco.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyevaa nguo ya bluu) akionesha jambo
wakati mchezo dhidi ya Mahakama na Tanesco ukiendelea. Kushoto ni Mkurugenzi
Msaidizi wa Utawala Stephen Magoha na kulia ni Mwenyekiti wa Mahakama Sports
Klabu Wilson Dede.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiteta jambo na Nahodha wa timu ya mpira wa miguu Seleman Magawa mara baada ya mechi kumalizika.
Picha ya pamoja kikosi cha mpira wa miguu toka Mahakama wakiwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisalimiana na timu ya Kamba (ME) toka Mahakama kabla ya mchezo wao dhidi ya Ikulu.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni