Jumamosi, 29 Aprili 2023

‘TUTUMIE MABARAZA YA WAFANYAKAZI KUTATUA CHANGAMOTO ZETU’

Na Francisca Swai-Mahakama, Musoma.

Mahakama Kanda ya Musoma imefanya Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi hivi karibuni uliloongozwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanania katika Kanda hiyo, Mhe. Frank Mahimbali kujadili masuala mbalimbali ya kiutumishi.

Akifungua Mkutano huo, Mhe. Mahimbali aliwaasa wajumbe wa Baraza kuwa wawazi na kuwasilisha hoja muhimu za kujenga ili kuboresha utendaji kazi. Aliwahimiza kutumia Mabaraza ya Wafanyakazi kutatua changamoto zinazowakabili wanapotekeleza majukumu yao ya kiutumishi.

“Wajumbe wote waliochaguliwa kuwawakilisha watumishi wenzao kutoka katika matawi, muwe wawazi kusema yale mliyotumwa ili kuyapatia ufumbuzi unaojenga na kuboresha mazingira ya kazi na kuleta umoja, upendo na mshikamano katika kazi,” alisema.

Akiongea katika Baraza hilo, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Mara, Bw. Hamis Mwisa aliwaeleza wajumbe kazi za Baraza, ikiwemo kuwashirikisha wafanyakazi wa Serikali katika utekelezaji wa shughuli za kiserikali kwa ushirikiano na uongozi.

Alitaja kazi zingine kama kuishauri Serikali juu ya ufanisi wa kazi na hatua zinazofaa kuchukuliwa ili kuhakikisha huduma zitolewazo zinaridhisha na zimo katika lengo la Taifa la kuleta maendeleo ya nchi, kuishauri Serikali juu ya mambo mengine muhimu yanayohusu maslahi na hali bora za wafanyakazi wa Serikali, kushauri juu ya miundo na masharti ya utumishi serikalini na kutoa ushauri katika matumizi ya fedha kufuatana na kasma.

Katibu Mwisa aliendelea kuwaasa watumishi wa ajira mpya na watumishi wote kujiunga na vyama vya wafanyakazi kwani vipo kisheria na vinafanya kazi kubwa ya kuwatetea katika masuala mbalimbali ikiwemo kuboresha maslahi, uonevu kazini na mengine.

Nao viongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma walioshiriki katika Baraza hilo ambao ni Naibu Msajili, Mhe. Frank Moshi na Mtendaji wa Mahakama, Bw. Festo Chonya, waliwaasa wajumbe na watumishi wote kuwa ili kuwepo na mazingira rafiki ya kazi ni muhimu kufanya kazi kwa kupendana, umoja na ushirikiano.

Walisema kuwa watumishi hutumia muda mwingi zaidi wakiwa kazini kuliko nyumbani, hivyo mazingira ya kazi yakiwa rafiki huweza kuwajenga kiafya, kisaikolojia na kuleta furaha.

Baadhi ya mambo yaliyojadiliwa katika Baraza hilo ni pamoja na Serikali kuboresha maslahi ya watumishi, michango ya asilimia 20 inayorudishwa kwenye matawi ifike kwa wakati, watumishi kulipwa malimbikizo ya mishahara kwa wakati na changamoto za watumishi kukaa katika kituo kimoja cha kazi kwa muda mrefu.

Katika Mkutano huo uliofanyika uchaguzi wa Katibu Msaidizi wa Baraza hilo ambapo Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Serengeti, Bi. Faraja Barakazi alichaguliwa kushika nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Bi. Alicia Bernado aliyepata uhamisho kutoka Mahakama Kuu Musoma kwenda Mahakama ya Wilaya Chato.  

Watumishi wa Kanda ya Musoma waliohudhuria Baraza la Wafanyakazi lililofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Musoma wakiimba kwa pamoja wimbo wa wafanyakazi (Mshikamano Daima) kabla ya ufunguzi wa Mkutano wa Baraza hilo.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Mahimbali akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi (hawako pichani) wakati akifungua Mkutano wa Baraza hilo.

Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma, Bw. Kandana Lucas ambaye pia ni Afisa Tawala, Mahakama Kuu Musoma akiwakaribisha wajumbe na waalikwa (hawako pichani) wa Baraza hilo.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Bw. Festo Chonya akisoma taarifa ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ndani ya Kanda wakati wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma lililofanyika Mahakama Kuu Musoma hivi karibuni.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Moshi akielezea mipango ya Kanda ya Musoma kuhusu matumizi ya TEHAMA wakati wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma lililofanyika Mahakama Kuu Musoma hivi karibuni.

Katibu Msaidizi wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma, Bi. Faraja Barakazi (aliyesimama) ambaye pia ni Afisa Tawala Mahakama ya Wilaya Serengeti akitoa neno la shukrani baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo.

Katibu wa TUGHE Mkoa wa Mara, Bw. Hamis Mwisa akifafanua umuhimu wa Mabaraza ya Wafanyakazi kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma lililofanyika Mahakama Kuu Musoma hivi karibuni.

Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi, Bw. Maulid Magoma (aliyesimama) akitoa hoja wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Musoma lililofanyika Mahakama Kuu Musoma hivi karibuni.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni