Na Faustine Kapama-Mahakama, Dar es Salaam
Watumishi wa Mahakama ya
Tanzania, Kanda ya Dar-es-Salaam, leo tarehe1Mei, 2023 wameungana na Watanzania
wengine kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi, inayojulikana kama Mei Mosi, inayosherekewa
kote duniani.
Maadhimisho hayo ambayo
mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Mwanahamisi Munkunda, yamefanyika
katika Uwanja vya Uhuru katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuhudhuriwa na maelfu
ya wananchi.
Pilikapilika za
maadhimisho hayo zilianza mapema asubuhi ambapo watumishi wa Mahakama
waliojitokeza kwa wingi waliungana na wananchi wengine katika eneo la Mnazi
Mmoja na baadaye kushiriki kwenye maandamano hadi kwenye Uwanja wa Uhuru.
Maandamano hayo
yaliyoongozwa na Bendi ya Jeshi la Magereza yalipita katika barabara ya
Nyerere, Keko na baadaye Uwanja wa Uhuru na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ambaye
alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makala.
Mbali na watumishi kupita
mbele ya mgeni rasmi kwenye maandamano hayo, magari ya Mahakama nayo yalikuwa miongoni
mwa magari kutoka taasisi na mashirika mbalimbali ambayo yalipita mbele yake,
likiwemo gari la Mahakama Inayotembea, ‘Mobile Court’, ambalo lilikuwa kivutio
kikubwa kwa wananchi.
Baada ya maandamano hayo,
ratiba ya maadhimisho hayo iliendelea, ikiwemo viongozi mbalimbali wa Chama cha
Wafanyakazi (TUCTA) na Serikali ya Mkoa walipata nafasi ya kutoa salamu.
Akizungumza katika
maadhimisho hayo, Mhe. Munkunda amewapongeza wafanyakaizi wote kwa kujitokeza
kwa wingi kushiriki kwenye maadhimisho hayo ambayo kwa mwaka huu wa 2023
yamebeba kauli mbiu inayosema, “Mshahara Bora na Ajira za Staha ni Nguzo kwa
Maendeleo ya Wafanyakazi, Wakati ni Sasa.”
Bendi ya Jeshi la Magereza ikiongoza maandamano hayo kukatisha mitaa mbalimbali hadi Uwanja wa Uhuru.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni