Jumanne, 2 Mei 2023

‘MFUMO ULIOBORESHWA KUONDOA MATUMIZI YA KARATASI, KUBEBA MAJALADA MKONONI’

Na Naumi Shekilindi-Mahakama, Simiyu

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga imeendelea kutoa mafunzo kuhusu Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri ulioboreshwa (e-case Management system) kwa watumishi na wadau wa Mahakama.

Safari hii mafunzo hayo yamefanyika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu yakiongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Warsha Ng’humu aliyeambatana na Afisa Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka Kanda hiyo, Bi. Nashilaa Mollel.

Katika mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibuni, Mhe. Ng’humu alisema mfumo huo ulioboreshwa umetajwa kuwa miongoni mwa mifumo bora itakayorahisisha utendaji kazi mahakamani katika kusajili na kumaliza mashauri kwa wakati.

“Mfumo huu ni mzuri ikiwemo kuondoa matumizi ya karatasi na ubebaji wa majalada ya mashauri, kwani kila kitu sasa kitafanyika kielectroniki,” Naibu Msajili alisema.

Naye Afisa TEHAMA aliongezea kuwa kila kitu kimerahisishwa katika mfumo huo tofauti na mfumo wa awali yaani (JSDS II). Aliosema ni mfumo rafiki ambao unakwenda kuondoa kabisa matumizi ya karatasi mahakamani.

“Kwa Mahakama, haya ni maboresho makubwa kuelekea Mahakama Mtandao, mfumo huu ni suluhisho katika upatikanaji haki kwa wakati. Mfumo huu umeunganishwa na mifumo mingine ya Mahakama kama mfumo wa ukusanyaji maduhuli ya Mahakama,” alisema Bi. Mollel.

Wakati wa mafunzo hayo, watumishi na wadau walioshiriki waliweza kuuliza maswali mbalimbali ili kupata uelewa zaidi wa mfumo huo kwani Mahakama inakwenda kwa kasi katika matumizi ya TEHAMA, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja wao kuufahamu.

 

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Warsha Ng’humu akitoa mada kuhusu mfumo huo.

Afisa TEHAMA Bi. Nashilaa Mollel akiwasilisha mafunzo juu ya utumiaji wa mfumo wa usimamizi wa mashauri (e- case management system).

Watumishi pamoja na wadau wakisikiliza kwa umakini mafunzo ya ‘e-case management system’ yaliokuwa yanatolewa na Afisa TEHAMA.

Watumishi na wadau wa Mahakama waliohudhuria mafunzo ya ‘e-case management system’ mkoani Simiyu wakiwa katika picha ya pamoja.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni