Jumanne, 2 Mei 2023

WATUMISHI WA MAHAKAMA SIMIYU MAMBO SAFI

·Mkuu wa Mkoa awakubali kwa kuchapa kazi

· Asema hajawahi kusikia harufu ya rushwa mahakamani

Na Naumi Shekilindi-Mahakama, Simiyu

Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Simiyu jana terehe 1 Mei, 2023 waliungana na Watanzania wengine kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo aliwamwagia sifa watumishi wa Mahakama kwa kazi nzuri wanayofanya katika kuwahudumia wananchi.

“Niwapongeze sana watumishi wa Mahakama Mkoa wa Simiyu kwa kazi nzuri mnayofanya. Toka nifike katika Mkoa huu sijawahi kusikia harufu ya rushwa mahakamani,” alisema alipokuwa anaongea na wananchi kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika wilayani Busega.

Kadhalika, Mkuu wa Mkoa alitoa salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa yupo pamoja na wafanyakazi wa Mkoa wa Simiyu na ataendelea kutoa ushirikiano kwa watumishi.

“Rais Samia pia ameahidi kuongeza ajira na kati ya ajira 21,000, Simiyu pia itanufaika na ajira hizo,” Mkuu wa Mkoa aliwaambia wananchi watumishi kutoka taasisi mbalimbali waliohudhuria maadhimisho hayo.

Mhe. Dkt. Nawanda aliahidi kutoa ushirikiano kwa Mwenyekiti wa TUCTA kuhakikisha watumishi wanapewa maslahi yao.

Mkuu wa Mkoa pia aliwashukuru wafanyakazi wote kwa ushirikiano wanaoumpa na kuomba kuendeleza ushirikiano huo sambamba na maagizo kwa wakuu wa idara kusimamia maslahi ya wafanyakazi ili kuleta tija katika utendaji kazi.

Maadhimisho hayo yalifunguliwa sala na dua kutoka kwa viongozi wa dini, ikafuatia risala fupi iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa TUCTA wa Mkoa, Bw. Kulwa Dwese, ambaye alielezea maslahi ya wafanyakazi kwa ujumla, hasa fedha za likizo na posho.

“Mheshimiwa mgeni rasmi, likizo na posho za watumishi hasa wa sekta ya elimu na afya ifike hatua sasa maslahi yao yaangaliwe kwani kuna watumishi wana zaidi ya miaka kumi hawajawahi kulipwa likizo wala posho,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda akihutubia wafanyakazi katika Mkoa huo kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani.

Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Simiyu waliohudhuria maadhimisho ya Mei Mosi Simiyu.

Wafanyakazi hodari na Afisa Tawala wa Mahakama wakiwa wameshika vyeti vyao ikiwa kama sehemu ya pongezi kutoka TUGHE.

Mahakimu Wafawidhi na Mtendaji wa Mahakama wakiwa katika maadhimisho hayo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni