Na
Mary Gwera, Mahakama-Mwanza
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma ametoa rai kwa Majaji nchini kuwa sehemu ya maboresho ya Mahakama
yanayoendelea kufanyika ili kila mmoja afahamu kwa kina kinachoendelea kwa
manufaa ya Mhimili huo na umma kwa ujumla.
Akizungumza leo tarehe 14 Aprili, 2023 na Majaji
hao wakati akiahirisha Kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya
kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025 kilichofanyika kwenye
Hoteli ya Malaika jijini Mwanza, Mhe. Prof. Juma amesema kwamba, suala la
maboresho ni endelevu hivyo ni muhimu kila mmoja kujihusisha nalo.
“Tunapozungumzia maboresho endelevu lazima kila
mmoja wetu aelewe kinachoendelea siyo kwa kuambiwa tu bali pia kwa kusoma, na kwa bahati nzuri nyaraka
nyingi sana za maboresho zipo na maswali mengi sana ambayo yanaulizwa kuhusu
maboresho zinapatikana kupitia tovuti na blogu ya Mahakama, hivyo
tunapotekeleza shughuli zetu za uondoshaji wa mashauri ni vizuri pia kuyaelewa
maboresho,” alisema Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Prof. Juma alipongeza jitihada mbalimbali zilizofanyika zenye kuleta maboresho ndani ya Mahakama huku akitaja baadhi ya Ofisi ndani ya Mhimili huo zikiwemo Kitengo cha Maboresho, Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri, Idara ya TEHAMA, Kamati ya Jaji Mkuu ya Kanuni na nyingine.
Amesema kwamba Idara/Vitengo/Kamati hizo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuchagiza maboresho hususani katika usimamizi wa matumizi ya teknolojia,
usimamizi wa mashauri, utungaji wa kanuni zaidi ya 75 zilizowezesha kurahisisha
baadhi ya taratibu za Mahakama na mengine.
Kadhalika, Jaji Mkuu amewataka Majaji kuzitumia
vyema kanuni zilizotungwa kuangalia namna bora ya kuzitumia kanuni mbalimbali
ili zisaidie kuleta maboresho katika huduma ya utoaji haki.
“Kamati ya Jaji Mkuu ya Kanuni ni moja ya Kamati
ambayo imefanya vizuri sana katika safari ya maboresho, zaidi ya kanuni 75
zimetungwa hivyo ni muhimu kuendelea kutumia kanuni hizo kuboresha zaidi huduma
za haki,” alisisitiza Mhe. Prof. Juma.
Katika kikao hicho
cha siku tatu (3) mada mbalimbali zimetolewa ambazo ni pamoja na taarifa ya hali ya utoaji
haki Mahakama ya Tanzania kwa mwaka 2022, TEHAMA, Maboresho ya huduma za
Mahakama na nyingine, kadhalika Maafisa hao wa Mahakama wamekubaliana kufanya
kazi kwa ushirikiano, kuendeleza matumizi ya TEHAMA, kuangalia namna ya
kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri vyote vikilenga kuboresha
huduma za upatikanaji haki kwa wananchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni