·Kasi ya kushughulikia mlundikano yashangaza
· Jaji Kiongozi azinyoshea kidole Mahakama za Hakimu Mkazi
Na Faustine
Kapama-Mahakama, Mwanza
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Mustapher
Siyani amewapongeza Majaji wa Mahakama ya Tanzania kwa kutekeleza kikamilifu
majukumu yao katika mnyororo mzima wa utoaji haki nchini, ikiwemo kuondosha
mlundikano wa mashauri.
Mhe. Siyani ametoa pongezi hizo leo tarehe 14
Aprili, 2023 kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma kufunga Kikao cha Tathmini ya Utendaji wa Mahakama na Mapitio ya Nusu ya
Kwanza ya Mpango Mkakati (2020/2021-2024/202)5 kilichokuwa kinafanyika jijini
hapa.
“Niwapongeze Majaji wote wakiongozwa na Majaji wa
Mahakama ya Rufani. Kazi iliyofanyika mwaka jana ni kubwa sana. Binafsi ninawasiwasi
kwa kasi hii ikiendelea kufikia mwaka 2025, Mahakama nzima itakuwa imeponya
kati ya magonjwa sugu, ikiwemo hili la ucheleweshaji wa mashauri,” amesema.
Jaji Kiongozi alitolea mfano wa Mahakama Kuu ya Tanzania
jinsi ilivyoshughulikia mlundikano wa mashauri kwa kipindi cha miaka mitatu
iliyopita ambapo kiwango kimeshuka kwa asilimia nane.
Alibainisha kuwa mwaka 2020, Mahakama Kuu ilikuwa na
mlundikano wa asilimia 15 ya mashauri yote na mwaka uliofuata wa 2021, kiwango
kikashuka hadi asilimia 11.7 na mwaka jana 2022, kiwango hicho kimeshuka tena mpaka
asilimia saba.
“Katika kipindi cha
miaka mitatu iliyopita, Mahakama Kuu imepunguza mashauri ya mlundikano kwa asilimia
nane, kutoka asilimia 15 mwaka 2020 hadi asilimia saba mwaka jana 2022. Kwa
hiyo, mimi sina wasiwasi hata kidogo, naamini mwaka huu maajabu mengine
yatatokea,” amesema.
Hata hivyo, Jaji
Kiongozi alieleza kuwa kupitia mada zilizowasilishwa wakati wa Kikao, bila shaka
washiriki watakuwa wameona maeneo Mahakama ya Tanzania imefanikiwa na maeneo
ambayo haikufanikiwa.
“Ingawa tunajivunia yale
ambayo tumefanikiwa kama taasisi, nguvu zetu sasa ni lazima zijielekeze kwenye
maeneo ambayo hatukufanikiwa, kama utekelezaji wa amri za Mahakama, hili ni
eneo ambalo linachangamoto na sababu ni nyingi ambazo ni mtambuka,” Mhe. Siyani
amesema.
Kadhalika, alibainisha pia
uwepo wa mashauri ya mlundikano kwenye Mahakama za Hakimu Mkazi, jambo ambalo
amesema lazima lifanyiwe kazi kwa sababu halikubaliki na anaamini Majaji Wafawidhi
wamesikia ni eneo linalohitaji usimamizi na ushirikishwaji wadau.
Jaji Kiongozi amesema kwa
Mahakama Kuu, anatumaini mapinduzi yaliyofanywa na Mahakama ya Rufani yataigwa.
Amesema kufanyika kwa Kikao hicho siyo tu kimetoa nafasi ya
kujadiliana mambo mbalimbali yanayohusu kazi na majukumu ya Mahakama, lakini
pia kimetoa fursa adhimu ya kufahamiana.
“Nimefurahi Kikao hiki
kimejumuisha Majaji wote. Kumekuwa na desturi ya kuwa na Majaji Wafawidhi peke
yake, lakini uwepo wa Majaji wote umewafanya kusikia kwa pamoja hali ya utendaji
kazi katika Mahakama kwa ngazi zote nchini na kupata fursa ya kutafakari
mchango wao kuelekea kwenye Mahakama ambayo haina mlundikano wa mashauri,” amesema.
Mhe. Siyani amebainisha
pia kuwa idadi ya Majaji wa Mahakama Kuu kwa sasa inaridhisha ukilinganisha na
miaka iliyopita. Amesema kuna vituo vingine vya Mahakama Kuu, ukiangalia idadi
ya mashauri yanayopokelewa kwa mwaka dhidi ya idadi ya Majaji waliopo vituo
hivyo havipaswi kuwa na mlundikano wa mashauri.
“Najua nitakuwa na fursa
wiki ijayo ya kuzungumza na Majaji Wafawidhi, jambo hili tutaliangalia ili ile
kasi ambayo ilikuwepo toka mwaka juzi 2020 iwe kubwa zaidi mwaka huu 2023,”
ameeleza Jaji Kiongozi.
Aidha, amesema taarifa
iliyowasilishwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma wakati
wa Kikao inaonyesha Majaji 43 wamefikia lengo lililokuwa limewekwa.
“Ni matumaini yangu
idadi hiyo itaongezeka zaidi mwaka huu na kwamba Mahakama Kuu haitageuka kuwa
Maktaba ya mlundikano, bali itakuwa Maabara ya mlundikano ambapo mashauri
yanashughulikiwa kwa haraka zaidi,” amesema.
Juzi tarehe 12 Aprili,
2023 alipokuwa anawasilisha mada, Msajili Mkuu aliwaeleza washiriki wa Kikao kuwa
Mahakama ya Tanzania imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji
wa majukumu yake ya utoaji haki kwa wananchi kwa mwaka 2022, hivyo kufanya dira
yake katika utoaji na kupatikana haki kwa wakati na kwa wote kuwa kweli.
Alisema
utendaji katika maeneo ya kiwango cha uodoshaji na kumaliza mashauri (case
clearance and disposal rate), mlundikano na muda ulivuka malengo mengi
yaliyowekwa katika Mpango Mkakati wa Mahakama na Mradi wa Maboresho ya Mahakama.
Mhe.
Chuma alieleza kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, utendaji wa
Mahakama ya Tanzania katika kazi zake za kimahakama umekuwa ukiimarika katika
ngazi ya kimahakama moja na kitaasisi kwa ujumla.
"Haya
ni matokeo ya mikakati iliyowekwa na Mahakama na kuungwa mkono na Serikali ikiwa
ni pamoja na kuongeza idadi ya maofisa wa Mahakama, kuondolewa vikwazo mbalimbali,
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na ushirikishwaji wa kimkakati
wa wadau," alisema.
Kadhalika,
alieleza kuwa mapitio ya mara kwa mara ya sheria, mipango ya kuondosha mashauri,
kujitoa na kujitolea kwa wafanyakazi na mabadiliko ya mtazamo ni miongoni mwa
sababu za mafanikio hayo.
Sehemu nyingine ya tatu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani (juu mstari wa kwanza na chini wa kwanza kushoto) ikimsikilia Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (hayupo katika picha). Wengine katika picha ya juu na chini ni Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (juu na chini) ikimsikilia Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (hayupo katika picha).
Sehemu nyingine ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (juu na chini) ikiwa katika Kikao hicho.
Sehemu nyingine ya tatu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (juu na chini).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni