Ijumaa, 14 Aprili 2023

MAFUNZO YA MFUMO WA USIMAMIZI WA MASHAURI YASHIKA KASI

 Na Mayanga Someke – Mahakama Kuu Sumbawanga

Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Sumbawanga imetoa mafunzo kwa Watumishi wake ya kuwapa uelewa juu ya utumiaji rafiki wa mfumo mpya wa usimamizi wa mashauri (e-Case Management System).

Akifungua mafunzo hayo jana tarehe 13 Aprili, 2023 katika ukumbi wa Mahakama Kuu Sumbawanga, Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bw. Emmanuel Munda alisema kuwa, baada ya mafunzo hayo, wao kama watumiaji wa ndani wa mfumo huo watakuwa tayari kutoa huduma bora zaidi na za haraka kwa wananchi.

“Ni imani yangu kuwa baada ya mafunzo haya, watumishi watakuwa na uelewa wa pamoja wa namna ya kutumia mfumo huo na hatimaye kurahisisha kazi na kutoa haki kwa wakati,” alieleza Bw. Munda.

Aliwakumbusha watumishi hao kwamba, Mahakama ipo katika utekelezaji wa mpango mkakati 2021/22-2024/25 na lengo ni kuhakikisha utoaji huduma ya haki unamlenga mwananchi. “Utekelezaji wa nguzo ya pili ambayo ni upatikanaji wa haki kwa wakati umejikita katika kutoa huduma za kuongeza ufanisi katika usikilizaji wa mashauri na kuboresha upatikanaji wa kumbukumbu na taarifa,” alisisitiza.

“Katika kutekeleza malengo hayo ya kimkakati, Mahakama imeona ni vema kuwekeza zaidi katika matumizi ya TEHAMA ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, hivyo tunapoanza mafunzo ya mfumo mpya ‘e-CMS’ niwaombe washiriki muwe na utayari wa kujifunza na kuelewa.” Alisema Bw. Munda.

Alisema kuwa, ujio wa mifumo hii ya kielektroniki inawataka watumishi wa Mahakama kuyaishi mageuzi na matumizi ya TEHAMA katika Mahakama, hivyo ni vizuri fikra za watumishi zilenge na kuyakubali mageuzi haya ili kwenda sambamba na maono ya viongozi wa Mhimili huo.

Akifunga Mafunzo hayo, naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Maira Kasonde aliwasihi watumishi wawe na utayari chanya wa kutumia mfumo huo ili kufikia muelekeo sahihi wa Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’.

Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri ulioboreshwa ‘Advanced e-Case Management System’ ni mfumo ambao umeboreshwa zaidi ya JSDS 1& 2 ambapo maeneo yaliyoboreshwa katika mfumo huo ni pamoja na ufunguaji wa mashauri, usikilizwaji na usimamizi wa mashauri kwa ujumla. Aidha mfumo huo umeunganishwa na kusomana na mifumo mingine  serikalini.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Sumbawanga, Bw. Emmanuel Munda (aliyesimama) akifungua mafunzo kwa Watumishi wa Mahakama Kuu, Hakimu Mkazi na Wilaya za Kalambo, Nkasi na Sumbawanga. Kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu-Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Maira Kasonde na kulia ni Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga, Mhe Kisasila Saguda.

Washiriki wakifuatilia mada ya 'Advanced e-Case Management System' iliyokuwa ikitolewa.

Naibu Msajili wa Mahakama (T) Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Maira Kasonde (aliyesimama) akitoa maelezo kuhusu Mfumo wa 'Advanced e-case Management System.'

(Taarifa hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama)

 


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni