Ijumaa, 14 Aprili 2023

MAHAKAMA DIVISHENI YA ARDHI, WADAU WAKUTANA

Na Dillon John-Divisheni ya Ardhi

Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, hivi karibuni ilifanya kikao na wadau kujadili namna bora ya kushughulikia migogoro ya ardhi inayohusisha mabenki na utatuzi kwa njia ya usuluhishi. 

Kikao hicho kilifanyika kwenye ukumbi wa Udzungwa wa Benki Kuu ya Tanzania na kuhudhuriwa washiriki wapatao 115 ambao ni wadau wa mashauri ya ardhi.

Akifungua kikao hicho, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani alisema kuwa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi imepata fursa adhimu ya kukutana na wadau muhimu katika utekelezaji wa majukumu yake ya msingi.

Jaji Kiongozi alieleza kuwa vikao vya namna hiyo vinatoa fursa ya kuwakutanisha wadau ambao kwa pamoja hujadili namna nzuri zaidi ya kuboresha shughuli za utoaji haki kwa wananchi.

Aidha, aliwasihi wadau waliohudhuria kikao hicho kushiriki kikamilifu kwa kusikiliza kwa makini na kujadili mada zitakazowasilishwa, kuibua mawazo yenye mlengo wa kuimarisha utendaji kazi sambamba na kuazimia mambo yatakayoongeza tija na ufanisi unaolenga kuboresha maisha ya wananchi.

Kwa upande mwingine, Mhe. Siyani aliupongeza uongozi na menejimenti ya Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi kwa maandalizi mazuri ya kikao hicho kilichohusisha idadi kubwa ya wadau kutoka nyanja mbalimbali za jamii,  wakiwemo viongozi kutoka taasisi za Serikali kama Wizara ya Ardhi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Wadau wengine waliohudhuria ni Mawakili wa Kujitegemea, viongozi wa dini, viongozi wa Serikali wa ngazi za Mitaa na Kata, Wenyeviti wa mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ya Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani pamoja na viongozi waliowahi kuhudumu kwenye Divisheni hiyo kwa wadhifa wa Jaji Mfawidhi na Mtendaji wa Mahakama. 

 Mhe. Jaji Kiongozi alitoa rai kwa vituo vingine vya Mahakama hasa Divisheni za Mahakama Kuu kuiga mfano wa Divisheni ya Ardhi. Alisema ni lazima Mahakama kujenga na kuimarisha mahusiano na ushirikiano na wadau ili kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kadhalika, Mhe. Siyani aliwasihi watumishi na wadau wote kutimiza majukumu na wajibu wao kwa weledi na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na sheria. Akisisitiza matumizi ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, Jaji Kiongozi alitoa mfano wa nchi ya Indonesia ambayo alisema imepiga hatua kubwa ambapo takribani asilimia 98 ya mashauri humalizika kwa njia ya usuluhishi.

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agnes Mgeyekwa aliwashukuru wadau na viongozi wote wa Mahakama kwa kuitikia wito wa kuhudhuria kikao hicho.

Alisisitiza kwamba Divisheni ya Ardhi inatambua umuhimu wa wadau katika kuboresha utekelezaji wa majukumu yake. Hivyo, aliahidi kuendelealea kuimarisha ushirikiano na ushirikishwaji wao. Mhe. Mgeyekwa aliwaomba kutoa maoni na ushauri wakati wowote.

Kipekee alitoa shukrani kwa kundi la washiriki lililojumuisha viongozi waliohudumu tangu kuanzishwa kwa Divisheni hiyo katika nyadhifa ya Jaji Mfawidhi na Mtendaji wa Mahakama. Majaji Wafawidhi waliowahi kushika wadhifa huo ni pamoja Rehema Kerefu (Jaji Rufaa), Issa Maige (Jaji Rufaa), Engela  Kileo (Jaji Rufaa Mstaafu), Richard Mziray (Jaji Rufaa Mstaafu) na Gadi Mjemmas (Jaji Mstaafu) ambao walihudhuria kikao hicho.

Katika kikao hicho mada zilizolenga kuwapa washiriki uelewa wa masuala ya kisheria ikiwemo namna bora ya kushughulikia mashauri ya ardhi yanayohusisha mabenki iliyowasilishwa na Wakili Gasper Nyika na utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa njia ya usuluhishi iliyowasilishwa na Wakili Abdallah Gonzi.

Katika mada yake, Wakili Nyika alisisitiza umuhimu wa sekta ya mabenki katika maendeleo ya uchumi wa wananchi na kuiomba Mahakama kushughulikia mashauri hayo kwa wakati ili kusisimua maendeleo ya wananchi. Aidha, aliwasisitiza washiriki kujielimisha kuhusu masuala na sheria za mabenki ili waweze kufanya maamuzi sahihi na kuepuka changamoto za kisheria zinazosababishwa na kukosa uelewa sahihi. 

Kwa upande wake, Wakili Gonzi aliwasihi Mawakili kujikita katika matumizi ya njia ya usuluhishi kutatua migogoro ili kuwapunguzia wananchi gharama na muda wa kufuatilia mashauri mahakamani. Alisistiza kwamba usuluhishi huondoa usumbufu usio wa lazima kwa Mahakama na kwa wananchi kwenda mahakamani kufuatilia mashauri, hivyo kujikita kwenye shughuli za maendeleo.

Baada ya mada hizo kuwasilishwa, washiriki walipata nafasi ya kuzijadili na walionesha kufurahishwa na mipango, malengo na mikakati mbalimbali iliyowekwa na Mahakama ya Tanzania katika kuboresha shughuli za utoaji haki kwa wananchi na kuboresha maisha ya watanzania.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Mustapher Siyani akizungumza wakati akifungua Kikao cha Wadau kilichoandaliwa na Mahakama ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agnes Mgeyekwa akitoa neno la shukrani.
Wakili Abdallah Gonzi akiwasilisha mada.
Wakili Gasper Nyika akiwasilisha mada.
Mshiriki akichangia mada.

Wadau mbalimbali wakifuatilia uwasilishaji wa mada.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mwanza).

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni