Na Emmanuel Oguda-Mahakama, Shinyanga
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Shinyanga wametakiwa kuyapa kipaumbele matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) katika kutekeleza jukumu la utoaji haki kwa wakati.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Seif Kulita wakati wa kikao
cha Baraza la Wafanyakazi Kanda kilichofanyika jana tarehe 27 Aprili, 2023 katika
ukumbi wa Mahakama Kuu.
Mhe. Kulita alisema kuwa, kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa
mara kwa mara na viongozi wa Mahakama ya Tanzania, matumizi ya TEHAMA mahakamani
hayaepukiki, hivyo ni muhimu yakapewa kipaumbele na kila mtumishi ili
kutekeleza adhma ya Mahakama ya kutoa haki kwa wakati kupitia TEHAMA.
“Kila mmoja anapaswa kubadilika na kuwa na nia ya
dhati katika kuwa sehemu ya mabadiliko kuelekea Mahakama Mtandao,” alisema Jaji
Kulita. Alisisitiza matumizi ya ‘video conferencing’ hasa kwa Mahakama ambazo
hazina magereza ili kupunguza gharama za kusafirisha Mahabusu kwenda mahakamani.
Jaji Kulita alitoa mifano kadhaa, ikiwemo namna TEHAMA
ilivyosaidia zoezi la kuondoa mashauri ya mlundikano katika Kanda ya Shinyanga,
hivyo kuwataka watumishi kuendeleza matumizi ya mifumo ya kielektroniki
inayoendelea kuboreshwa na Mahakama ya Tanzania ili kila mmoja awe sehemu ya mchango
katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama (2020/2021 – 2024/2025).
Kadhalika, Jaji Kulita aliwataka watumishi wote wa
Mahakama Kanda ya Shinyanga kama walivyowasilisha taarifa ya kutokuwa na
mashauri ya mlundikano kutozalisha mashauri ya aina hiyo ili kutimiza azimio lililowekwa
katika Kanda ya Shinyanga tarehe 7 Februari, 2022.
Naye Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu
na Afya (TUGHE) Mkoa wa Shinyanga, Bw. Ramadhani Pangara, aliipongeza Mahakama
Kuu Kanda ya Shinyanga kwa kuwa na vikao vya Baraza ambavyo vinawapa nafasi
watumishi kujadili mambo mbalimbali yanayohusu utumishi wao, haki na stahiki
zao pamoja na changamoto zinazowakabili.
Alisema kwa kiasi kikubwa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga
inajitahidi kuzitatua baadhi ya changamoto hizo na zile ambazo zipo nje ya
uwezo wake huwasilishwa kwa viongozi wakuu wa Mahakama kwa ajili ya utatuzi.
Wakati huo huo, aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athumani Matuma, ambaye amehamishiwa Kanda ya
Tabora amewaaga Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kutoka Kanda hiyo baada ya
kupata nafasi ya kuhudhuria kikao hicho.
Mhe. Matuma aliwashukuru watumishi wa Kanda ya
Shinyanga kwa ushirikiano katika kipindi chote alichofanya nao kazi tangu
alipoteuliwa kushika wadhifa huo Desemba 2021. Aliwataka watumishi hao
kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jaji Mfawidhi mpya kama walioutoa kipindi cha
uongozi wake.
“Nawaomba muendelee kufanya kazi kwa bidii na
kutoruhusu mashauri ya mlundikano kama tulivyoazimia, nitafurahi sana kama
mtaendelea kushirikiana, kupendana na kufanya kazi kwa bidii zaidi,” alisema
Mhe. Matuma.
Kikao cha Baraza la Wafanyakazi Kanda ni jukwaa linalokutanisha watumishi mbalimbali wa Mahakama kujadili hali ya utendaji kazi pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili. Katika kikao hicho, wajumbe waliwachagua Bw. Robert Nchimbi kuwa Katibu wa Baraza Kuu Kanda ya Shinyanga na Bw. Shomari Mrisho kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa kutoka Kanda hiyo.
Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Seif Kulita
akisisitiza jambo wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Shinyanga.
Katibu
wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Mkoa wa Shinyanga, Bw.
Ramadhan Pangara akichangia hoja wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi
Kanda.
Mtendaji
wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Bi. Mavis Miti akifuatilia kwa makini hoja
zilizokuwa zikiwasilishwa katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi Kanda ya
Shinyanga.
Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athumani Matuma akiongea na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Shinyanga.
Sehemu
ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Shinyanga wakiwa katika kikao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni