Na Evelina Odemba Mahakama Morogoro
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim
Hamis Juma jana tarehe 27 Aprili, 2023 alizungumza na watumishi wa Mahakama ya
Tanzania, Kanda ya
Morogoro na kuwahimiza kujiendeleza kielimu
ili kukabiliana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia ambayo inakuwa kwa kasi
kote duniani.
Mhe. Prof. Juma alisisitiza watumishi kuwa
na jitihada binafsi za kujisomea na wanaweza kufanya hivyo hata kwa kutumia
vifaa vyao vya mawasiliano, ikiwemo simu janja ambazo asilimia kubwa ya
watumishi wanazimiliki.
“Nafikilia Mahakama tutawatumia walioko
karibu kuwapa elimu na mafunzo ya mara kwa mara watumishi wetu, nadhani TAWJA
ni miongoni mwa tutakaowatumia kwani wapo karibu sana,” alieleza Jaji Mkuu. TAWJA
ni Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza katika tukio hilo alisisitiza watumishi
wa Mahakama kuwa watulivu wakati masuala mbalimbali ya kiutumishi yakishugulikiwa.
Aliwaasa kuepuka kutoa taarifa wasizokuwa na uhakika nazo.
Kadhalika, Prof. Ole Gabriel alipongeza
jitihada zilizofanywa na Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro kwa kuchimba
kisima cha maji safi ambacho kitaenda kuwa msaada mkubwa kwakuwa na maji ya
uhakika, hatua itakayopunguza gharama. Aliahidi kununua pampu kubwa
itakayowezesha kusukuma maji.
Awali, wakati akisoma taarifa ya utendaji
kazi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul
Ngwembe alieleza kuwa watumishi wa Mahakama katika eneo lake wanafanya kazi kwa
bidii na hutumia muda wa ziada kufanya kazi.
Alisema uwepo wa Kituo Jumuishi cha Utoaji
Haki umepunguza gharama na wamekuwa wakipokea pongezi mbalimbali toka kwa wananchi
ambao wananufaika na uwepo wa huduma ya Mahakama Kuu kwenye Kanda ya Morogoro.
Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Wilbard Chuma alisema kuwa wataendelea kutoa mafunzo ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa watumishi wa Mahakama ili kuwajengea
uwezo katika kazi. Alisema mafunzo hayo yatatolewa kwa njia ya moja kwa moja na
kwa njia ya Mtandao.
Katika kikao hicho, Jaji Mkuu aliambatana
na Majaji wa Mahakama ya Rufani, akiwemo Mhe. Lilian Mashaka na Mhe. Omar
Makungu, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe
Chaba na Mhe. Gabriel Malata, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Sylivester
Kahinda na viongozi wengine kutoka Kanda ya Morogoro.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.Ibrahim Hamis Juma (aliyevaa suti ya blue) akizungumza na viongozi mbalimbali wa Mahakama, akiwemo Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania (aliyeonesha mgongo), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (kulia), Jaji Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija (wa pili kushoto), Jaji Mahakama ya Rufani, Mhe. Lilian Leonard (kushoto) na anayefuatia ni Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba (aliyesimama nyuma).
(Habari
hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni