Na Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba
Mahakama Kanda ya Bukoba
jana tarehe 27 Aprili, 2023 iliendesha mafunzo kuhusu mfumo wa kuratibu
mashauri ulioboreshwa wa kielektroniki unaojulikana kama Advanced Case
Management System (e-CMS) ili kuwajengea uelewa wa pamoja Mahakimu ili waweze
kutekeleza vyema jukumu la utoaji haki kwa wananchi.
Mafunzo hayo ambayo yalihusisha
Mahakimu wa Mahakama za Wilaya zote za Mkoa wa Kagera yalihudhuriwa pia na Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Imakulata Banzi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi
wa mafunzo hayo, Mhe. Banzi aliwaasa washiriki wote kuuelewa mfumo huo ambao utasaidia
katika utendaji kazi na kurahisisha mwenendo wa usikilizaji wa mashauri.
“Mafunzo haya yanahitaji
uelewa wa pamoja ili kuendelea kutimiza jukumu la utoaji haki kwa wote na kwa
wakati. Hivyo, nawaasa msikilize kwa makini kwani mfumo huu utawasaidia sana wakati
mnapotekeleza jukumu la kutoa haki kwa wananchi,” Jaji Mfawidhi alisema.
Wito kama huo ulitolewa
pia na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe Odira
Amworo ambaye aliwahimiza washiriki hao wa mafunzo kusikiliza kwa makini ili
kuelewa vizuri namna mfumo huo unavyofanya kazi kufuatia maboresho makubwa yaliyofanyika.
Akitoa mafunzo hayo,
Afisa Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Bukoba, Bw. Ahmed Mbilinyi alisema mfumo huo umeboreshwa kufuatia changamoto
zilizokuwa zinajitokeza wakati wa matumizi ya mfumo wa awali unaojulikana kama Judicial
Statistics Dashboard (JSDS II).
Alisema kwa sasa mfumo huo ulioboreshwa utakuwa na ufanisi zaidi. Alielezea mfumo huo wa e-CMS wa upokeaji na uratibu wa mashauri umeboreshwa kuanzia shauri linapofunguliwa mpaka shauri linapofikia hatua ya kutolewa maamuzi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe Immaculata Banzi akitoa neno la ufunguzi
katika mafunzo ya mfumo ulioboreshwa wa kuratibu mashauri.
Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe Odira Amworo (aliyesimama) akimkaribisha Jaji Mfawidhi Banzi (katikati) kutoa neno la ufunguzi.
Mahakimu wa Mkoa wa Kagera (juu na picha mbili chini) wakisikiliza neno la ufunguzi kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe Immaculata Banzi.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni