·Mfuko wakubali kuboresha Maktaba wa Divisheni ya
Kazi
Na Mwanaidi Msekwa-Mahakama Kuu, Kazi
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni
ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina hivi karibuni alitembelea ofisi za Mfuko wa
Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ikiwa miongoni mwa ziara zake kuwatambua wadau
mbalimbali wanaohusika moja kwa moja na masuala ya kazi.
Jaji Mfawidhi alifanya ziara katika ofisi za Mfuko huo
zilizopo Kijitonyama Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kujitambulisha na
kubadilishana uzoefu kwa kuwa shughuli zake zinauhusiano wa karibu na kazi
zinazofanywa na Mahakama yake.
Baada ya kufika katika ofisi za WCF, Mhe. Dkt. Mlyambina
alifanya mazungumzo na mwenyeji wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa
Wafanyakazi, Dkt. John Mduma. Katika mazungumzo yao, viongozi hao waligusia
majukumu, mafanikio na changamoto zinazoikabili Mahakama Kuu, Divisheni ya
Kazi.
Jaji Mfawidhi aliainisha baadhi ya changamoto, ikiwemo
ukosefu wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa ajili ya
Maktaba, mahitaji ya Sheria za Mfuko na mafunzo kuhusu sheria hizo kwa Majaji,
Naibu Wasajili, Wasaidizi wa Sheria wa Majaji na Wasuluhishi na Waamuzi wa migogoro
katika Tume ya Usuluhishi na
Uamuzi (CMA).
Naye Dkt. Mduma, akizungumza katika tukio hilo, alimshukuru
Jaji Mfawidhi kwa kumtembelea ofisini kwake ambapo alionesha mwitikio chanya
katika kufadhili ununuzi wa vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya Maktaba kama vile kompyuta
na vifaa vingine vya kieletroniki pamoja na kufadhili mafunzo yaliyoombwa.
Katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Mlyambina aliongozana na viongozi wengine wa kutoka Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, akiwemo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Enock Kassian.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni
ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Dkt. John Mduma (katikati). Kushoto ni Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Enock Kassian.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama,
Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni