·Apokea ofisi rasmi kutoka kwa Jaji Amour
Na Amani Mtinangi- Mahakama. Tabora
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Athuman Matuma jana terehe 17 Mei, 2023
amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Jaji
Mfawidhi wa Mahakama katika Kanda hiyo, Mhe. Amour Khamis na kuahidi kuelekeza nguvu kubwa kuhakikisha mashauri
ya mlundikano yanamalizika.
Mhe. Matuma alisema uwiano wa
mashauri anaoachiwa ni mzuri ukilinganisha na idadi ya Majaji na Mahakimu waliopo.
Alitolea mfano wa Mahakama Kuu yenye Majaji watatu ambayo kuna mashauri 393 ukilinganisha
na Mahakama Kuu Shinyanga yenye takriban mashauri 600.
“Kituo hiki kina mashauri
machache ukilinganisha na nilipotoka katika Mahakama Kuu Shinyanga. Kwa mujibu
wa taarifa zilizopo, hapa kuna mashauri 393 ukilinganisha na takriban mashauri
600 ya Shinyanga,” alisema.
Mhe. Matuma alionyesha kuridhishwa
na ushirikiano alioupata kwa kipindi kifupi alichokaa Tabora na kuahidi kuendeleza
mazuri yote aliyoyakuta.
Akizungumza wakati wa kukabidhi
ofisi hiyo, Mhe. Amour alishukuru ushirikiano alioupata kwa watumishi na wadau
wote katika kipindi alichokuwa akihudumu katika kituo hicho.
Alimhakikishia Jaji Matuma
kuwa watumishi wanaohudumu katika kituo hicho wana ari, moyo na juhudi ya
kufanya kazi na kusifu hatua mbalimbali na ubunifu uliofanywa na viongozi.
“Watumishi wa kituo hiki ni
wachapakazi, weledi na wana ari ya kufanya kazi, ni watendaji wasiohitaji
kusimamiwa. Naamini watakuwa msaada sana kwako kwenye utekelezaji wa majukumu
yako,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Msajili
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Niku Mwakatobe alimshukuru Mhe.
Amour kwa uongozi wake mzuri na wa kuigwa, huku akimkaribisha Mhe. Matuma
katika Kanda ya Tabora.
Naye Mtendaji wa Mahakama Kanda
ya Tabora, Bw. Ginaweda Nashon alisema Jaji Amour alikuwa mwalimu na msaada kwake
tangu alipofika katika Kanda hiyo, alimpokea na kufanya naye kazi vizuri.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Uyui, Mhe. Tausi Mongi (aliyesimama) akisema neno wakati wa makabidhiano hayo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni