Na Faustine Kapama-Mahakama
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan ameteua Majaji sita wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa Majaji wa
Mahakama ya Rufani.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais Ikulu, Bi Zuhura Yunus leo tarehe 18 Mei, 2023 imesema uteuzi huo umeanza
tangu tarehe 28 Aprili, 2023 na wateule hao wataapishwa tarehe itakayotangazwa
baadaye.
Walioteuliwa ni Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala
ya Familia Temeke, Mhe. Zainab Goronya Mruke na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania
na Mkuu wa Shule ya Sheria Tanzania, Mhe. Dkt. Benhajj Shabaan Masoud.
Taarifa hiyo inawataja wateule wengine ni aliyekuwa
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora ambaye kwa sasa
anahudumu katika Kanda ya Shinyanga kwa nafasi hiyo, Mhe. Amour Said Khamis na
Jaji wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dar es Salaam, Mhe. Leila Edith Mgonya.
Wengine ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson John Mdemu na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agnes Zephania Mgeyekwa.
Uteuzi huo unaongeza idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani kutoka 26 waliopo hivi sasa hadi 32.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni