Na Evelina Odemba
Mahakama Morogoro
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania waliopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro jana tarehe 16 Mei, 2023 walipatiwa elimu ya usalama na afya mahali pa kazi na wataalamu kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na kuaswa kuwa na matumizi sahihi ya jengo hilo.
Wataalamu hao walifanikiwa kukagua maeneo ya utendaji kazi, ikiwemo miundombinu ya umeme na maji ambayo inatumika katika jengo hilo na kushauri masuala kadhaa ya matumizi sahihi ya vitendea kazi bora vilivyopo.
Baada ya ukaguzi huo, Mtaalamu wa OSHA, Bw. Renatus Qalqal alisema kituo hicho kina mazingira bora na salama ya kufanyia kazi na kimedhibitiwa hatari ambazo zinaweza kutokea kwa watumiaji. Alishauri kuongezwa kwa baadhi ya alama ambazo zitasaidia kumwongoza mtumiaji ambaye ni mgeni.
Naye Mhandisi Mariam Ndaskoy alitoa elimu kuhusu masuala ya msingi ya matumizi ya umeme na kusisitiza kuwatumia wataalamu kutoka OSHA kwa ajili ya ukaguzi.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe, ambaye alifungua na kufunga zoezi hilo, alisema elimu iliyotolewa na wataalamu hao imekuwa na manufaa kwa watumishi wa Mahakama kwakuwa wataitumia mpaka majumbani.
Aliongeza kuwa kwa sasa Mahakama inaboresha miundombinu yake, ikiwemo ujenzi wa majengo mapya ya kisasa. Mhe. Ngwembe aliwaomba OSHA kutosita kutembelea na kutoa elimu ili watumiaji wawe salama na majengo hayo yaweze kutumika kwa muda mrefu.
“Tutaendelea kuwatumia wataalamu mbalimbali ili watupe ujuzi na maarifa, leo tumepokea elimu toka OSHA na mwaka 2022 tuliipata kutoka Jeshi la Zimamoto. Hakika elimu hizi zinatusaidia sana, tukumbuke kuwa mtu anayekimbilia elimu ni mwelevu na sisi tunataka kuwa welevu,” alisema na kuongeza kuwa atashangaa kusikia uwepo wa mtumishi asiyependa kujifunza.
Baada ya zoezi hilo, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bw. Ahamed Ng’eni aliwashukuru wataalamu wa OSHA kwa shughuli waliyofanya na kuwahakikishi kuwa wameyapokea maboresho yaliyoelekezwa ambayo yanatakiwa kufanyika ndani ya jengo hilo.
Alisema ushauri uliotolewa utafanyiwa kazi, ikiwemo kulitunza vizuri jengo hilo ili liendelee kufaa kwa matumizi kwa muda mrefu. Mtendaji huyo alisema ujenzi wa kituo hicho umetumia kiasi kikubwa cha fedha, hivyo hawatakuwa tayari kuona linaharibika.
Tangu kuanzishwa kwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro mwezi Oktoba 2021, uongozi umekuwa ukitoa elimu ya sheria kwa watumishi na wananchi kwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali.
Mpaka sasa wamefanikiwa
kutoa elimu ya Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili watumishi waweze kwenda
na mabadiliko ya teknolojia, huduma kwa wateja, zimamoto, masuala ya fedha toka
kwa wataalamu wa Benki ya CRDB na elimu ya usalama mahali pa kazi toka OSHA.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni