Jumatano, 24 Mei 2023

JAJI MDEMU AWAAGA WATUMISHI WA MAHAKAMA SINGIDA; AWAASA KUSHIRIKIANA

Na Eva Leshange- Mahakama, Singida

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu amewaaga watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida baada ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani (T) hivi karibuni.

Akizungumza na watumishi hao kwenye hafla ya kumuaga iliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida hivi karibuni, Mhe. Mdemu aliwashukuru kwa kufanya kazi nao pamoja kwa ushirikiano.

“Nawashukuru sana watumishi wenzangu kwa kukaa pamoja muda wote nikaona ni vyema kuwaaga, changamoto katika kazi zipo na hazifanani hivyo zisitufanye kujiona hatufai tutatue changamoto zetu tusiwe watu wa kulalamika” alisema Jaji Mdemu.

Aidha, Mhe. Mdemu amesisitiza ushirikiano, kufanya kazi kwa umoja na kuishi vizuri na watu kwani unaweza ukahawa kituo fulani na baadae ukahamia kituo kingine na ukakutana na watu uliowahi kufanya nao kazi. Kadhalika amesisitiza kutokukata tamaa katika kazi, kufanya kazi kwa juhudi na kujiendeleza ili kufika mbali zaidi.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi, Hakimu Mkuu Mahakama ya Mwanzo Utemini, Mhe Joyce Shilla alimshukuru Jaji Mdemu kwa kipindi chote walichofanya kazi nae kwani alikua ni zaidi ya kiongozi kwao kwakuwa wamejifunza mengi kutoka kwake. Na vilevile amemtakia heri na baraka katika Majukumu yake mapya.

Mhe. Mdemu ni miongoni mwa Majaji sita walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani. Majaji hao waliapishwa jana tarehe 23 Mei, 2023 na Rais, Mhe. Dkt Samia Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu (kulia)  akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida (hawapo katika picha) wakati akiwaaga baada ya kuteuliwa hivi karibuni kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani (T). Kulia ni Jaji wa Mahamama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Suleiman Haji Hassan.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama Singida wakimsikiliza Mhe. Mdemu (hayupo katika picha) wakati wa hafla ya kumuaga. Wa kwanza kulia  ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Singida, Mhe. Ushindi Swallo, wa pili kulia ni Mtendaji Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Bw. Yusuph Kasuka.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama Singida wakimsikiliza Mhe. Mdemu (hayupo katika picha) alipokuwa akizungumza wakati wa hafla ya kumuga. Wa kwanza kulia ni Mtendaji Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Bw. Yusuph Kasuka.  

Hakimu Mkuu Mahakama ya Mwanzo Utemini, Mhe Joyce Shilla (aliyesimama) akitoa neno la shukrani  kwa niaba ya watumishi wengine kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Gerson Mdemu wakati wa hafla ya kumuaga iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida.

(Taarifa hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni