Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama
Shirika la Umoja wa
Mataifa la Kuzuia Dawa za Kulevya na Uhalifu ((UNODC) linaendesha mafunzo
maalum kwa watumishi wa Mahakaka ya Tanzania, hususan Majaji na Mahakimu kuwaongezea
uelewa kuhusu Sheria ya Bahari na Hukumu.
Mafunzo hayo ya siku tano
ambayo yanafanyika katika Hoteli ya Protea Mkoa wa Dar es Salaam yalifunguliwa
na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta
Opiyo.
Akizungumza wakati
anafungua mafunzo hayo, Mhe. Dkt. Opiyo alitoa shukrani zake za dhati kea UNDC
kwa msaada wao kufanikisha mafunzo hayo.
“Natambua juhudi kubwa za
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Jaji Dkt. Paul Kihwelo, ambaye
ameiongoza timu ya Chuo hicho katika kuandaa mafunzo haya. Kujitolea kwake na
utaalamu wake umekuwa muhimu, tunashukuru sana kwa michango yake,
"alisema.
Jaji huyo alieleza pia
kuwa wamekuwa na bahati ya kuwa na Jaji Maurice Kamga, Jaji wa Mahakama ya
Kimataifa ya Sheria ya Bahari, ambaye amekuwa mwanachama mashuhuri wa Mahakama
hiyo tangu tarehe 1 Oktoba, 2020.
“Uwepo wake hapa unasisitiza umuhimu wa
mafunzo haya na umuhimu wa masuala tutakayojadili. Tuna hamu ya kujifunza
kutokana na ujuzi na uzoefu wake mkubwa katika nyanja hiyo,” alisema.
Jaji Opiyo alibainisha
kuwa katika mtazamo wa Tanzania, Sheria ya Bahari inahusu mfumo wa kisheria
unaosimamia haki na wajibu wa nchi katika matumizi na usimamizi wa bahari ya
dunia na rasilimali zake.
Alisema Tanzania, ikiwa
ni nchi ya pwani inafungwa na Mkataba wa
Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari (UNCLOS), ambao ni makubaliano ya msingi
ya kimataifa yanayosimamia masuala ya bahari.
Tanzania, kama mataifa
mengine ya pwani, ina haki na mamlaka fulani juu ya eneo lake la maji, ambayo
yanaenea hadi maili 12 kutoka kwa msingi wake. Ndani ya ukanda huu, Tanzania
ina mamlaka kamili, ikiwa ni pamoja na haki ya kudhibiti na kunyonya rasilimali
zilizo hai na zisizo hai.
Jaji Opiyo alisema pia kuwa
zaidi ya eneo lake la maji, Tanzania ina eneo la kipekee la kiuchumi (EEZ)
ambalo linaenea hadi maili 200 kutoka katika msingi wake.
"Katika EEZ,
Tanzania ina haki huru ya kuchunguza, kunyonya, kuhifadhi na kusimamia
maliasili, hai na isiyo hai, katika safu ya maji na juu au chini ya
bahari," alisema.
Jaji Opiyo alieleza zaidi
kuwa Tanzania pia inastahili kupata haki katika upanuzi wa chini ya maji wa
ardhi yake. Alisema kuwa eneo hilo linaenea zaidi ya EEZ katika hali fulani,
kwa kuzingatia jiolojia ya bahari.
“Tanzania, kama mshirika
wa UNCLOS, inatekeleza kanuni za ulinzi wa mazingira ya baharini, usimamizi
endelevu wa uvuvi na uhifadhi wa viumbe hai vya baharini. Nchi ina jukumu la
kuzuia na kudhibiti uchafuzi wa mazingira katika maji yake, "alisema.
Jaji Opiyo pia alieleza
kuwa Tanzania ikiwa ni nchi ya mwambao wa Afrika Mashariki, inakabiliwa na
matukio ya uhalifu mbalimbali wa baharini, ukiwemo uharamia, uvuvi haramu,
biashara ya dawa za kulevya, biashara haramu ya binadamu na biashara haramu.
"Ni muhimu kutambua
kwamba Tanzania, kama nchi nyingine nyingi, inachukulia kwa uzito uhalifu huu
wa baharini na inashirikiana na washirika wa kimataifa, kama vile mashirika ya
kikanda, nchi jirani, na vyombo vya sheria vya kimataifa, kupambana na vitendo
hivi haramu na kudumisha usalama wa baharini." alisema.
Hii ni mara ya pili chini
ya mradi wa Global Maritime Crime Programme (GMCP), kwa Shirika hilo kufadhili
mafunzo ya aina hiyo kwa Majaji na Mahakimu wa Tanzania.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo akizungumza wakati anafungua mafunzo hayo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo (kulia) akiwa na Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Sheria ya Bahari, Mhe. Maurice Kamga.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (wa kwanza hadi wa tatu kutoka kushoto) wanaohudhuria mafunzo hayo.
Mchanganyiko wa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakimu wanaohudhuria mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni