Na Tiganya Vincent-Mahakama, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuongeza jopo
jingine la Majaji wa Mahakama ya Rufaa ili kuendelea kupunguza mrundikano wa
mashauri.
Ametoa kauli hiyo leo
tarehe 23 Mei 2023 wakati wa hafla fupi ya kuwaapisha Majaji sita wa Mahakama
ya Rufani iliyofanyika Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma kufuatia uteuzi alioufanya
hivi karibuni.
Mhe. Dkt.Samia alisema
lengo ni kufikisha Majopo ya Majaji wa Mahakama ya Rufani 10 badala ya tisa (9),
hatua hiyo itasaidia kuharikisha utoaji haki kwa wananchi katika ngazi ya
Mahakama ya Rufani.
"Napenda kukupongeze
Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kupata timu mpya ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na
kila nitakapokuwa nikiteua nitaongeza idadi ya wanawake ili kufikia wastani wa
hamsini kwa hamsini," alisisitiza.
Aliongeza kuwa sanjari ya
kuongeza Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani pia ataongeza Majaji wa Mahakama
Kuu wapya kwa lengo la kuhakikisha utoaji wa haki kwa wananchi unafanyika kwa
wakati.
Naye Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema uteuzi na uapisho alioufanya
Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan umeweka historia kwa ongezeko la idadi ya Majaji wa Mahakama ya
Rufani.
Alisema kuwa kabla ya
Rais Samia kuingia madarakani, Majaji wa Rufani walikuwa hawazidi 16 na
alipoingia aliongeza na kufikia 25 na uapisho mpya umefanya wafikie Majaji wa
31 hapa nchini.
Mhe. Prof. Juma alisema
hatua hiyo umesaidia Mahakama ya Rufani kuongeza Majopo ya Majaji wa Mahakama
ya Rufani kutoka saba hadi kufikisha Majopo tisa ambapo kwa wastani kila Jopo hukaa
Majaji watatu, au watano, au saba kutokana
na shauri husika linalosikilizwa.
Alisema faida ambayo
Mahakama imeipata kutokana na uteuzi huo ni kupungua kwa mzigo wa mashauri
ambao kila jopo lilikuwa likiubeba ambapo kwa wastani yalikuwa mashauri 805 na
sasa yatafikia 626.
Aidha, Jaji Mkuu aliwataka
Majaji kubadili mtazamo ikiwemo kuangalia matumizi ya usuluhushi kwa baadhi ya
mashauri, ikiwemo ya biashara. Amesema hatua hiyo itapunguza mrundiko wa
mashauri ambayo yangeweza kumalizika kwa mazungumzo.
Naye Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson alisema wako tayari
kufanya marekebisho kwenye maeneo ambayo ni kikwazo katika utoaji wa haki ili
wananchi wapate haki kwa wakati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni