Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan leo tarehe 23 Mei, 2023 amewaapisha Majaji sita wapya wa Mahakama
ya Rufani aliowateua hivi karibuni.
Hafla hiyo ya uapisho imefanyika katika Ikulu ya
Chamwino Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa wa Serikali
na Mahakama. Majaji hao wamekuwa viongozi wa kwanza kuapishwa na Rais Samia
kwenye jengo jipya la Ikulu tangu lilipozinduliwa tarehe 20 Mei, 2023.
Majajı hao ni aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Kituo
Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Zainab Goronya Mruke na aliyekuwa Jaji
wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dar es Salaam, Mhe. Leila Edith Mgonya.
Wengine ni aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania
na Mkuu wa Shule ya Sheria Tanzania, Mhe. Dkt. Benhajj Shabaan Masoud na aliyekuwa
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Amour Said
Khamis.
Kadhalika, aliapishwa aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson John Mdemu na aliyekuwa Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agnes Zephania
Mgeyekwa.
Viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson na Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe, Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas
Ndumbaro, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Jaji wa
Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Mhe. Mustapher Mohamed Siyani.
Kulikuwepo pia na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
watumishi mbalimbali wa Mahakama wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel na ndugu na jamaa wa viongozi hao walioapishwa.
Tukio hilo pia liliambatana na uapisho wa Mwenyekiti
wa Baraza la Maadili, Mhe. Rose Teemba, ambaye ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu
ya Tanzania. Baada ya uapisho huo, viongozi hao walikula kiapo cha uadilifu
kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya
Rufani, Mhe. Sivangilwa Mwangesi.
Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao, Rais
Samia aliahidi kuendelea kuiwezesha Mahakama kwa kuipatia nguvu kazi ya kutosha
ili kuharakisha mchakato mzima wa utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Dkt, Samia alisema ataongeza jopo moja la Majaji
wa Mahakama ya Rufani ili yafikie kumi (10), hatua itakayosaidia kuongeza kasi
ya usikilizaji wa mashauri na utoaji wa uamuzi.
Alielezea furaha yake baada ya kuona wale aliowateua
kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani ni miongoni mwa wale aliowateua kuwa Majaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na wamekuwa
wakitimiza majukumu yao kikamilifu.
“Nakupongeza Jaji Mkuu kwa kupata timu mpya. Kwa majaji
wapya, hongereni sana kwa kupata uteuzi huu na kuapa. Kuna Majaji hapa niliwapandisha
mwenyewe kutoka huko walikokuwa kwenda Mahakama Kuu na leo wale wale nawaapisha
kwenda Mahakama ya Rufani. Hii inanipa faraja kundi hili linachapa kazi sawa sawa,”
alisema.
Naye Waziri Mkuu aliwaeleza Majaji hao kuwa Watanzania
wanamategemeo makubwa kutoka kwao na wanahamu ya kutendewa haki katika mahitaji
yao mbalimbali. “Sisi hatuna mashaka na nyinyi, utendaji wenu uliotukuka
tunauona, uadilifu na uaminifu katika kufanya kazi za utoaji haki,” alisema.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge alieleza kuwa kama mwakilishi
wa wananchi wanatamani kuona hukumu zinatolewa kwa haraka ili wapate haki yao.
Alieleza kuwa Bunge litakuwa tayari kuzifanyia marekebisho sheria zile
zinazoleta changamoto katika utendaji wa Mahakama ili wananchi wapate haki zao
haraka.
Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mkuu wa Tanzania
alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia kwa kuiongezea nguvu kazi
Mahakama katika upande wa Mahakama ya Rufani, kwani ongezeko la Majaji hao
linaenda kupunguza mzigo wa kila jopo katika kusikiliza na kuamua mashauri.
Mhe. Prof. Juma aliwakumbusha Majaji hao majukumu yao
katika Mahakama ya Rufani ambayo ni kusikiliza na kuamua mashauri, hivyo
akawahimiza kutekeleza kazi hizo kwa wakati ili wananchi wapate haki zao na pia
kuchochea uchumi.
Rais Samia aliwateua Majaji hao sita tarehe 28 Aprili,
2023, hivyo kuongeza idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani kutoka 25 waliokuwepo
hadi 31, bila kujumlisha Jaji Mkuu.
Mhe. Zainab Goronya Mruke akiapa.
Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani wakiwa katika ukumbi Ikulu ya Chamwino Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni