Jumatatu, 22 Mei 2023

KAMISHNA NYANDUGA AIPONGEZA MAHAKAMA KWA UBORESHAJI HUDUMA

-Atoa rai kwa Taasisi nyingine za Kisheria kuiga mfano wa Mhimili huo

Na Mary Gwera, Mahakama

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wakili Bahame Tom Nyanduga ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kupiga hatua katika uboreshaji wa huduma zake hususani katika matumizi ya TEHAMA.
 
Akizungumza hivi karibuni jijini Dodoma katika kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania, Wakili Nyanduga alisema kwamba, katika Sekta ya Sheria nchini Mahakama imepiga hatua kubwa kimaboresho.

“Naomba nichukue nafasi hii kuipongeza Mahakama kwa jitihada za dhati katika uboreshaji wa huduma zake,” alisema.

Aliongeza kwa kutoa rai kwa Mhimili huo kutangaza maboresho yake hata kwa Taasisi nyingine za Haki ili nao waweze kwenda sambamba na kasi ya Mahakama ya uboreshaji huduma na hatimaye huduma ya utoaji haki iweze kuwafikia wananchi kwa urahisi.

Miongoni mwa maboresho yaliyofanywa na Mahakama ni pamoja na kuongezeka kwa kasi ya uondoshaji wa mashauri kutoka asilimia 78 mwaka 2021 hadi kufikia 84 mwaka 2022, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya majengo yake, kuongezeka kwa uwazi na uwajibikaji, uanzishwaji wa huduma ya Mahakama zinazotembea (Mobile Court services) na mengine.

Akiwasilisha mada katika kikao hicho, Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma alisema kuwa kiwango cha umalizaji wa mashauri kimeongezeka kutoka asilimia 99 kwa mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 106 mwaka 2022. Aliongeza kuwa, hilo linaenda sambamba na kupungua kwa mlundikano wa mashauri kutoa asilimia 11 kwa mwaka 2021 na kufikia asilimia 6 kwa mwaka 2022 na asilimia 3 kwa mwaka huu.

Naye, Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema Mahakama imepata mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs) sita na kuongeza kwamba, kwa sasa Mahakama ipo katika maandalizi ya awamu ya pili ya ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs) tisa (9) pamoja na kuanza kwa ujenzi wa Mahakama za Wilaya 15.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. 

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania.

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wakili Bahame Tom Nyanduga akizungumza katika kikao cha Baraza kuu la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.
Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wakili Bahame Tom Nyanduga akizungumza katika kikao cha Baraza kuu la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma. Kulia ni Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na kulia kwake ni Katibu wa Baraza hilo, Bw. Ezra Kyando.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis (katikati), Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Ezra Kyando (kushoto) na kulia ni Katibu Msaidizi wa Baraza la Wafanayakazi Mahakama ya Tanzania, Mhe. Christina Mlwilo wakimsikiliza Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wakili Bahame Nyanduga wakati alipokuwa akizungumza katika kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mahakakama kilichofanyika hivi karibuni.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama ambao pia ni Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania wakimsikiliza Kamishna ya Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wakili Bahame Nyanduga (hayupo katika picha) alipokuwa akizungumza kwenye kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni