Na Stephen Kapiga-Mahakama, Mwanza.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe.
Dkt. Ntemi Kelekamajenga amewahimiza watumishi katika Kanda hiyo kufanya kazi katika
kada zaidi ya moja, hatua itakayosaidia kupambana na upungufu wa rasilimali
watu sehemu za kazi.
Mhe.
Kelekamajenga alitoa wito huo jana tarehe 3 Mei, 2023 alipokuwa anaendesha
kikao cha menejimenti ya Mahakama katika Kanda hiyo inayojumuisha Mikoa ya
Mwanza na Geita katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki
Mwanza.
“Tatizo
la uhaba wa watumishi ni kilio kwa kila Mahakama zilizowasilisha taarifa zao za
utendaji na kuonesha changamoto ya upungufu wa watumishi, hivyo mkifanya kazi
zaidi ya moja kutasaidia kupambana na tatizo hili badala ya kuegemea kwenye
kada moja tu,” alisema.
Kadhalika,
Jaji Mfawidhi aliwahimiza wajumbe wa kikao hicho kujitahidi kila wakati kutumia
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA
katika kazi zao za kila siku kwani kwa sasa ndipo Mahakama inapoelekea kwenye Mahakama
Mtandao.
Mhe.
Dkt. Kelekamajenga pia alizungumzia suala la motisha kwa watumishi. Aliwaomba
wajumbe hao wa menejimenti kama viongozi kwenye maeneo yao kutoa motisha kwa
watumishi waliochini yao, hatua itakayoongeza morali ya kufanya kazi.
“Napenda
pia muone umuhimu wa kutoa motisha kwa watumishi ambao wapo chini yenu ili
kuweza kuwajengea morali ya kazi. Kuna aina nyingi za motisha kama ambavyo
wenzetu wa Ukerewe katika taarifa zao wameonesha namna walivyoweza kutembelea
mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro, hii inaweza kuinua molari ya
watumishi katika maeneo yenu,” alieleza.
Katika
hatua hatua nyingine, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza imebuni fomu laini maalumu
itakayokuwa inatumika kurejesha taarifa ya huduma anayopatiwa mteja katika Mahakama
hiyo.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Mhe. Monica Ndyekobora
aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho namna fomu hiyo itakavo fanya kazi.
“Fomu
hii tumeipa jina la “please rate me” ambayo mteja atatoa mrejesho wa huduma
aliyopewa na mtumishi na kuweza kuonesha kama ameridhishwa na huduma au la na
nini ushauri wake juu ya mtumishi aliyempatia huduma hiyo,” alisema.
Mhe. Ndyekobora alifafanua kuwa wanategemea kuanza kuutumia mfumo huo watakaponunua kishikwambi ambacho kitakuwa katika dirisha la kutolea huduma ndani ya Mahakama hiyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kelekamajenga(katikati) akieleza jambo kwa
wajumbe wa kikao cha menejimenti kilichofanyika jana tarehe 3 Mei 2023 kwenye ukumbi
wa mikutano katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza. Kushoto kwake ni
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mhe. Chiganga Mashauri na kulia
ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Mwanza Bw. Tutubi Mangazini.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Mwanza, Mhe. Chiganga Mashauri akieleza jambo wakati wa uchangiaji wa
mawasilisho ya taarifa za utendaji kazi kutoka katika Mahakama mbalimbali za Kanda
hiyo.
Sehemu ya wajumbe wa kikao
cha Menejimenti Mahakama Kanda ya Mwanza (juu na picha mbili chini) wakifuatilia kwa makini mawasilisho ya
taarifa za utendaji kazi kutoka katika vituo mbalimbali vya Mahakama zilizopo
katika Mikoa ya Geita na Mwanza.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni