Alhamisi, 4 Mei 2023

WATUMISHI WA MAHAKAMA RUKWA WASHIRIKI MAANDAMANO YA MEI MOSI 2023

Na Mayanga Someke-Mahakama, Sumbawanga

Wafanyakazi wa Mahakama Mkoa wa Rukwa hivi karibuni walijumuika na watumishi  wengine katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi), ambayo yalifanyika katika Uwanja wa Nelson Mandela uliopo katika Manispaa ya Sumbawanga.

Maadhimisho hayo yalianza kwa maandamano ya wafanyakazi kuanzia katika Ofisi ya Chama cha Walimu (CWT-RUKWA) kuelekea uwanja wa Nelson Mandela. Katika maandamano hayo, wafanyakazi wa taasisi na idara mbalimbali ikiwemo Mahakama walishiriki.

Kauli mbiu ya Siku ya Wafanyakazi mwaka 2023 ni “Mishahara Bora na Ajira zenye Staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi, Wakati ni Sasa”.  Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Queen Sendika.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Amiri Mruma alijumuika na wafanyakazi wa Mahakama katika kuadhimisha sherehe hizo. Viongozi wengine wa Mahakama walioshiriki ni Jaji wa Mahakama Kuu Sumbawanga, Mhe. Abubakar Mrisha, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda hiyo, Mhe. Maira Kasonde na Mtendaji wa Mahakama Kuu Sumbawanga, Bw. Emmanuel Munda.

Vilevile, wafanyakazi bora wa Mahakama walitangazwa na kupewa zawadi zao.Wafanyakazi hao ni Msaidizi wa Ofisi, Bi. Atupelile Konga kutoka Mahakama Kuu ya Sumbawanga na Katibu Mahsusi Daraja la Kwanza wa Mahakama Hakimu Mkazi Sumbawanga, Bi. Esther Kahale.

Wengine ni Katibu Mahsusi Daraja la Pili wa Mahakama ya Wilaya Nkasi, Bi. Lulu Aswile, Msaidizi wa Ofisi Mkuu wa Mahakama ya Mwanzo Mpui, Bw. Paskali Kiteta na Mlinzi Mkuu wa Mahakama ya Mwanzo Mwimbi, Bw.Zenos Kapufi.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa alizungumzia suala la kikokoto kuwa wataendelea kuomba na kushawishi mamlaka husika ili kufanyika marekebisho kwa vile jambo hilo lipo kisheria.

Suala hili la kikokoto lipo kisheria, hivyo kama viongozi tutaendelea kuomba na kushawishi mamlaka za juu kuliangalia upya,” alisema.

Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Rukwa wakiwa kwenye maandamano siku ya Mei Mosi.

Viongozi wa Mahakama walioshiriki maadhimisho hayo, akiwemo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Amiri Mruma (wa pili kulia) na Jaji wa Mahakama Kuu Sumbawanga, Mhe.Abubakar Mrisha ( wa kwanza kulia).


Mfanyakazi bora wa Mahakama Kuu Sumbawanga, Bi. Atupelile Konga akikabidhiwa cheti na pesa taslimu na Mkuu wa Mkoa, Mhe. Queen Sendiga.


Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Rukwa wakiwa kwenye uwanja wa Mandela kwenye sherehe za Mei Mosi.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni