·Mwakilishi atua mahakamani na mzigo wa vitabu vya sheria
Na Faustine Kapama-Mahakama, Dar es Salaam
Msaidizi Mwandamizi wa Mawasiliano na Usimamizi wa
Habari wa ILO Ofisi ya Dar es Salaam, Bi. Nasikiwa Berya, akiwa na makasha ya
vitabu hivyo aliwasili mahakamani hapo saa saba mchana na kupokelewa na
mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina.
Mara baada ya kutia sahihi kwenye kitabu cha wageni,
Mhe. Dkt. Mlyambina aliongozana na mgeni wake kwenye ukumbi uliokuwa umeandaliwa
kwa ajili ya makabidhiano ya vitabu hivyo, tukio lililoshuhudiwa na Majaji wote
wa Divisheni, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo, Mhe. Katarina Mteule na Mhe. Biswalo Mganga.
Wengine waliohudhuria tukio hilo ni Naibu Msajili Mfawidhi,
Mhe. Said Ding’ohi, Naibu Msajili, Mhe. Enock Cassian, Mtendaji, Bw. Samson
Mashalla, watumishi kutoka Divisheni hiyo wakiwemo viongozi wa Kamati ya Elimu
ya Ndani na mwakilishi kutoka Maktaba ya Mahakama, Bw Salum Tawani.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Mhe. Dkt. Mlyambina alisema kuwa tukio
hilo ni hatua muhimu katika kutafuta haki ndani ya maeneo yao na kulipongeza Shirika
hilo kwa msaada huo waliotoa na kujitolea kwa ajili ya kuendeleza hitaji la
kazi zenye staha na haki ya kijamii duniani kote.
"Kujitolea kwa ILO katika kuimalisha viwango vya kazi na kukuza haki
na usawa za ajira kumeleta mafanikio makubwa kwenye maisha ya wafanyikazi kote
ulimwenguni na maendeleo ya jamii yenye utaratibu. Tunashukuru sana kwa
ushirikiano na usaidizi wao katika kuimarisha uwezo wa Mahakama yetu ya Kazi,”
alisema.
Jaji Mfawidhi alieleza kuwa mchango huo wa vitabu unawakilisha utajiri wa
maarifa na ujuzi katika uwanja wa sheria za kazi. Alisema vitabu hivyo vitatumika
kama nyenzo muhimu kwa Majaji, Wasaidizi wa Kisheria wa Majaji, Wataalamu wa
Sheria na Watumishi wa Mahakama ili kuwawezesha kuongeza uelewa wao wa sheria
za kazi, viwango vya kimataifa vya kazi na sheria za kesi husika.
"Hii bila shaka itachangia katika utoaji wa haki kwa ufanisi katika Divisheni
yetu ya Kazi. Vitabu hivi vitachangia jukumu muhimu katika kujenga uwezo na
ukuzaji wa taaluma ndani ya mfumo wa Mahakama. Kwa kupanua upatikanaji wetu wa
fasihi ya kisheria, ILO imetuwezesha kukuza utamaduni wa kuendelea kujifunza na
kuimarisha ujuzi,” alisema.
Alieleza pia kuwa kitendo cha Shirika hilo kuiwezesha Mahakama ya Kazi
rasilimali zinazohitajika kunasisitiza umuhimu wa sheria za kazi kama njia ya
kulinda haki za wafanyakazi, kukuza uhusiano mzuri na kuchangia maendeleo ya
taifa.
Hivyo, alitoa shukurani zake za dhati kwa watumishi katika Shirika hilo waliojitolea
na kufanya kazi bila kuchoka ili kufanikisha mchango huo, akiwemo Mkurugenzi wa
ILO wa Afrika Mashariki, Ofisi ya Dar es Salaam anayemaliza muda wake, Mhe.
Wellingston Chibebe.
Naye Bi. Berya,
akizungumza baada ya kukabidhi vitabu hivyo, alishukuru uongozi kwa kuendelea
kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Mahakama hiyo na ILO na kuahidi
kuendeleza ushirikiano kati ya pande zote mbili.
Tukio la kukabidhi vitabu
hivyo limekuja muda mchache baada ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kukabidhi
vitabu vingine vinavyohusu sheria za kazi na fidia katika Divisheni hiyo.
Matukio hayo yote mawili
ni matunda yanayotokana na ziara alizozifanya hivi karibuni Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina kwenye taasisi
hizo ili kuendeleza uhusiano na kubadilishana uzoefu namna ya kutua migogoro ya
kazi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina.(kushoto) akimkaribisha ofisini kwake Msaidizi Mwandamizi wa Mawasiliano na Usimamizi wa Habari wa ILO Ofisi ya Dar es Salaam, Bi. Nasikiwa Berya baada ya kuwasili katika Mahakama hiyo jana terehe 3 Mei, 2023 kukabidhi vitabu mbalimbali vya masuala ya sheria za kazi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina.(katikati) akiwa na mgeni wake, Msaidizi Mwandamizi wa Mawasiliano na Usimamizi wa Habari wa ILO Ofisi ya Dar es Salaam, Bi. Nasikiwa Berya. Kushoto ni Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bw. Samson Mashalla.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni