Jumatatu, 8 Mei 2023

KANZIDATA YA KUSAJILI WATEJA YALETA MATOKEO CHANYA KITUO JUMUISHI TEMEKE

 ·Wananchi 910 wanufaika kwa siku

 Na Mujaya Mujaya-Kituo Jumuishi, Temeke.

Kanzidata ya Usajili wa Taarifa za Wateja (Customer Management Database) inayotumika kujisajili kidigitali katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke imeleta matokeo chanya, ikiwemo kupata takwimu sahihi za wananchi wanaofika kupata huduma katika Mahakama hiyo.

Hayo yalibainishwa na Jaji Mfawidhi wa Kituo hicho, Mhe. Zainabu Goronya katika Kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano mahakamani hapo kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji.

Mhe. Goronya alibainisha kuwa kwa sasa idadi ya wateja wanaohudumiwa kituoni hapo imefikia watu 910 kwa siku, idadi inayodhihirisha kuwa wananchi wametambua umuhimu wa huduma zinazotolewa katika Mahakama hiyo.

Kanzidata hiyo ilibuniwa na kutengenezwa na Afisa Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Kituo hicho, Bi. Amina Said ambapo kwa sasa wateja wote husajiliwa kidijitali getini kabla ya kuingia mahakamani kupata huduma.

Inaelezwa kuwa kanzidata hiyo ilibuniwa ili kuondoa changamoto za awali, ikiwemo kukosa takwimu za muda wanaotumia wananchi tangu wanapoingia mahakamani hadi wanapotoka ili kuweza Kituo hicho kujitathmini na kuweka mikakati madhubuti.

Tangu kuanzishwa kwa kanzidata hiyo mwezi Agosti 2022, jumla ya wateja 106,916 wamesajiliwa. Kati ya hao, wanaume ni 51,280 na wanawake ni 55,636. Kanzidata hiyo inarekodi yenyewe (automatic recording) siku na muda alioingia mteja, muda aliotoka pamoja na muda aliotumia kupata huduma kituoni hapo.

Vile vile inatoa takwimu za wananchi wenye mahitaji maalum kama vile wazee, watu wenye ulemavu, watoto na akina mama wanaonyonyesha ili wanapoingia mahakamani hapo waweze kupewa kipaumbele.

Katika kikao hicho, Baraza pia lilibainisha mafanikio mengine kadhaa yaliyopatikana, ikiwemo kuokoa gharama mbalimbali kupitia usikilizaji wa mashauri na usomaji wa hukumu au uamuzi kwa njia ya Mtandao.

Kadhalika, Kituo kimefikia makubaliano na chama cha mabenki kuhusu nyaraka zinazohitajika katika mashauri ya mirathi, hivyo kupelekea uwepo wa mahitaji yanayofanana baina ya mabenki, malipo ya mirathi kufanyika kwa wakati na kuboresha chumba cha kunyonyeshea watoto.

Vile vile, Kituo kimeendelea kutoa elimu kwa wateja kupitia maigizo, televisheni na vyombo vya sauti (PA system) na kuendesha vikao vya watumishi kila Ijumaa ili kubaini na kutatua changamoto mbalimbali.

Baraza liliazimia kuendelea kukabiliana na changamoto ya kutofungwa kwa mashauri ya mirathi, ikiwemo kuwafuatilia wasimamizi wa mirathi kwa kutumia anuani zao za makazi au kuwatangaza kwenye magazeti ili wafike mahakamani kufunga mirathi zao.

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke,
Mhe. Zainabu Goronya akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Kituo hicho, Mhe. Martha Mpaze akifafanua jambo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya katika Kituo Jumuishi hicho, Mhe. John Msafiri akichangia hoja.
Mkaguzi wa Ndani na Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi katika Kituo Jumuishi cha masuala ya Familia Temeke, Bwn. Mujaja Mujaya akichangia jambo.

Msaidizi wa Ofisi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Bi. Queen Mwakubombaki akisajili mteja kidijitaji. 

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wakiwa kwenye kikao. 

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni