·Mahakama yamwamuru kuchapwa viboko 12
·Mwathirika kulipwa milioni nne fidia
Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha
Mahakama ya Wilaya Kibaha imemhukumu Dereva wa Halmashauri ya Wilaya Kibaha, Fadhili Hai (57) kifungo cha miaka arobaini (40) jela na kuchapwa viboko 12 kwa kumbaka binti yake mwenye mtindio wa ubongo na kumsababishia ujauzito.
Kadhalika, Mahakama imemwamuru Dereva huyo kulipa fidia ya millioni nne (4,000,000/=). Adhabu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Judith Lyimo baada ya kumtia hatiani mshitakiwa kwa kosa hilo ambalo alilitenda kinyume na kifungu 158(1)(b) and (2) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Akisoma hukumu katika kesi hiyo, Hakimu Lyimo alisema kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa na pande zote mbili, Mahakama imeridhika upande wa mashtaka umedhibitisha pasi kuacha shaka mshitakiwa alitenda kosa hilo.
“Ushahidi wa mkemia ulioletwa na upande wa mashtaka unaonyesha vipimo alivyopima vinathibitisha mtoto aliyezaliwa ni wa mshitakiwa,” alisema. Katika shauri hilo, upande wa mashtaka ulileta mashahidi saba.
Hakimu Lyimo alibainisha kuwa ushahidi uliotolewa na shahidi mmoja kuwa mwathirika wa kosa hilo ana mtindio wa akili uliungwa mkono na Daktari ambaye alielezea jinsi hali yake ambayo kuna wakati anakua sawa na kuna wakati anakua hajielewi.
“Hivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba wakati mwathirika anamweleza shahidi namba mbili (jina lake limehifadhiwa) kufanyiwa kitendo kibaya na baba yake alikuwa katika hali ya kawaida,” alisema.
Katika maombolezo yake kupitia wakili wake Mwanaisha Ally, Mshitakiwa aliomba kupunguziwa adhabu kwa kuwa ni kosa la kwanza na ana ugonjwa wa moyo. Kadhalika, mshitakiwa huyo aliomba huruma ya Mahakama kwa kuwa ana familia inayomtegemea.
Awali, upande wa mashtaka
ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Bi. Gladness Mchami uliieleza Mahakama kuwa kwa
nyakati tofauti mwaka 2021, mwathirika alimtembelea mshtakiwa ambaye ni baba
yake mzazi na kumkuta akiwa peke yake.
Mshitakiwa alitumia nafasi hiyo kumbaka binti hiyo na kusababisha ujauzito. Mshitaka aliposomewa shitaka hilo alikana, hivyo kuulazimu upande wa mashtaka kuita mashahidi saba, akiwemo Daktari na Nesi aliyekuwa anamhudumia mwathirika.
Shitaka hilo lilifunguliwa mwaka 2021 katika Mahakama hiyo. Kabla ya kuanza kusikilizwa, upande wa mashtaka uliomba kuliondoa ili wasubiri mwathirika ajifungue kuwezesha mtoto kuchukuliwa vipimo vya vina saba (DNA).
Baada ya mtoto kuzaliwa, upelelezi ulifanyika ikiwemo kuchukuliwa vipimo hivyo, hatua iliyopelekea kesi hiyo kufunguliwa upya mwezi Februari, 2023.
Wakati wa kusikiliza shauri hilo, mwathirika hakuweza kutoa ushahidi. Upande wa mashtaka uliiambia Mahakama kuwa mwathilika hakuweza kutoa ushahidi kutokana na hali yake hubadilika badilika kila wakati.
Katika hali ya kujiridhisha na jambo hilo, Mahakama ilielekeza upande wa mashtaka kumleta mwathirika huyo mahakamani na baadaye kuridhika kuwa hakuwa na uwezo wa kujieleza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni