Na. Emmanuel Oguda-Mahakama, Shinyanga
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga wametumia vyema mapumziko ya mwisho wa juma hivi karibuni kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na kujionea vivutio mbalimbali katika hifadhi hiyo maarufu hapa nchini.
Watumishi hao wakiongozwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Bi. Mavis Miti wamejionea vivutio hivyo vinavyopatikana katika hifadhi na kustaajabu jinsi wanyama wanavyoweza kuishi chini ya Bonde kubwa la ‘Crater’ au Caldera kitu ambacho kinawipa hifadhi hiyo umaarufu ya Duniani.
Watumishi hao ambao wengi wao hawajawahi kufika katika hifadhi hiyo, wameelezea furaha yao baada ya kufurahia mandhari nzuri ya asili inayopatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro. “mtumishi huyo alisema uzuri wa hifadhi hii ni wa kipekee na inauoto wa kuvutia sana” alisikika mtumishi huyo.
Watumishi hao walijionea aina mbalimbali za Wanyama wanaopatikana katika hifadhi hiyo kama Simba, Tembo, Pundamilia na wengine, pamoja na vivutio vingine kama ziwa Magadi linalopatikana chini kabisa ardhini ndani ya hifadhi hiyo na wanyama aina ya kiboko wanaopatikana ndani ya ziwa hilo.
Mbali na kutembelea hifadhi hiyo, watumishi hao walipata nafasi ya kutembelea eneo la kufuga nyoka lililopo Arusha maarufu kama “Snake Park” na kupata maelezo ya aina mbalimbali za nyoka wanaopatikana katika eneo hilo na baadhi yao walipata fursa ya kuwashika nyoka ambao hawana madhara kwa binadamu.
Akiongea kwa niaba ya watumishi, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Bi. Mavis alisema kuwa, watumishi hao wameamua kwenda Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro kama sehemu ya kujifunza na pia kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kuhamasisha utalii wa ndani.
“Tutaendelea kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii
kwa kadri tunavyopata nafasi kujionea namna nchi yetu ilivyobarikiwa kuwa na
vivutio vingi ambavyo havipatikani maeneo mengi Duniani’’ alisema Bi. Mavis.
Sehemu watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga wakiwa kwenye picha ya pamoja mbele ya lango kuu la hifadhi walipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro hivi karibu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni