·Mahakama ya Mwanzo yapokea ushahidi kutoka Kenya, Mikoani
·Zaidi ya shilingi 1,000,000 za Kitanzania zaokolewa siku moja
Na Amina Saidi-Kituo Jumuishi, Temeke
Katika kutimiza azma ya utoaji haki kwa wakati,
Mahakama ya Mwanzo katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke leo
tarehe 9 Mei, 2023 imepokea ushahidi wa mashahidi wanne, mmoja kutoka Kisumu
Kenya kwa njia ya Mkutano Mtandao katika kesi inayohusu mirathi.
Ushahidi huo umetolewa mbele ya Hakimu Mkazi, Mhe. Nakijwa
Kachua katika Shauri la Mirathi Na. 531 la mwaka 2023 kuhusu marehemu Idrisa
Omary, huku muombaji usimamizi wa mirathi akiwa ni Bw. Omary Idrisa.
Inaelezwa kuwa mashahidi hao, akiwemo Bi. Khadija
Idrisa kutoka Kenya walishindwa kufika mahakamani kutokana na majukumu ya kazi,
ukosefu wa nauli na fedha za kujikimu, hali iliyopelekea Hakimu Kachua kutoa
amri ya shauri hilo kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
Miongoni mwa mashahidi waliosikilizwa kwa njia hiyo watoto
wa marehemu, akiwemo Bw. Athumani Idrisa kutoka Mkoa wa Songea, ambaye aliunganishwa
kutokea Mahakama ya Wilaya Songea.
Wengine ni Bw. Hashimu Idrisa kutoka Mkoa wa Mwanza, aliyeunganishwa
kutokea Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na Bw. Ibrahimu Idrisa kutoka Mkoa wa
Tanga, aliyeunganishwa kutokea Mahakama Kuu Kanda ya Tanga.
Akizungumza baada ya kumaliza kusikiliza shauri hilo, Mhe.
Kachua amewashukuru Maafisa Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama
Kanda ya Tanga na Mwanza na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Songea
kwa ushirikiano walioutoa kufanikisha zoezi hilo.
Amesema zaidi ya shilingi millioni moja za Kitanzania
(1,000,000/=) zingeweza kutumika kugharamia usafiri, chakula pamoja na malazi
endapo mashahidi wote wanne wangesafiri hadi Dar es Salaam kutoa ushahidi
katika shauri hilo.
Aidha, mashahidi hao kwa nyakati tofauti wameisifu na
kuishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kuwaokolea gharama kupitia teknolojia hiyo kwani
wameweza kutoa ushahidi wao vizuri na kumsikiliza Hakimu kwa umakini bila
changamoto yoyote.
Shauri hilo limeahirishwa hadi tarehe 15 Mei, 2023 kwa
ajili ya uamuzi.
Jengo la Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke ambapo shauri
hilo limesikilizwa.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni